Prime
Diarra awagawa mabosi Yanga

Muktasari:
- Lakini, wakati maisha yakiwa hivyo pale Jangwani, kule Msimbazi wako katika hatua za mwisho mwisho za mikakati ya kumalizana na Waarabu wa RS Berkane kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kila kitu kikitarajiwa kuwa hadharani baada ya dakika 90 za jioni ya Jumapili hii.
VIUNGA vya Jangwani mambo yanaonekana kana kwamba yamepoa, kikosi cha Yanga kikiwa mawindoni katika viwanja vya mazoezi kujiwinda na michezo iliyobaki kumalizia msimu huu wa Ligi Kuu Bara na fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Lakini, wakati maisha yakiwa hivyo pale Jangwani, kule Msimbazi wako katika hatua za mwisho mwisho za mikakati ya kumalizana na Waarabu wa RS Berkane kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku kila kitu kikitarajiwa kuwa hadharani baada ya dakika 90 za jioni ya Jumapili hii.
Hata hivyo, huku nyuma Yanga inaendelea na mkakati wa kuuza mastaa wa kikosi hicho na sasa staa mwingine ambaye anapasua vichwa vya mabosi wa klabu hiyo ni kipa Djigui Diarra.
Taarifa za Diarra ni kwamba ana hesabu za kutaka kuachana na klabu hiyo akishinikiza imuuze, lakini maombi yake yamewagawa mabosi wake wa juu.
Diarra bado ana mkataba na Yanga akiwa anaendelea kumfukuza kwa karibu kipa wa Simba Moussa Camara katika clean sheet za Ligi Kuu wakitofautiana moja tu, Camara akiwa na 16 na kipa huyo wa Yanga akiwa na 15 hadi sasa huku timu wanazochezea zikichuana katika mbio za ubingwa.
Kuna makundi mawili yameibuka ndani ya Yanga hasa kwa mabosi ambapo kundi la kwanza ni lile linalosema kipa huyo anayeitumikia timu hiyo kwa msimu wa nne tangu alipotua Agosti 2021 akitokea Stade Malien ya Mali, aruhusiwe kuondoka kama itapatikana timu ya kumnunua kwa fedha ndefu.
Kundi hili la kwanza linaona kipa huyo, ni kama anaendelea kushuka taratibu akiwa kama anapoteza morali ya kufanya kazi kwa nguvu.
"Hawa wanaona kama Diarra alipoteza tuzo msimu uliopita, lakini hata msimu huu hakuanza sawasawa, labda huku mwishoni ndio ameamka," amesema bosi huyo.
Kundi la pili ni lile linalopata wasiwasi kwamba endapo kipa huyo ataondoka watakuwa na mbadala wa maana wa kuziba nafasi yake mwenye ubora sawa na Diarra.
"Wengine tunaona wasiwasi kwa kuwa bado hatuonyeshwi mtu muafaka ambaye kama tutamruhusu Diarra kuondoka nani atachukua nafasi yake na tukasema kweli huyu ni mtu muafaka kwa hiyo bado hatujapata muafaka."
Diarra ndani ya msimu mitatu aliyoitumikia Yanga amefanikiwa kuchukua tuzo ya Kipa Bora mara mbili mfululizo kabla ya kupokonywa tuzo hiyo msimu uliopita na Mkongomani, Ley Matampi aliyekuwa kipa wa Coastal Union.
Kipa huyo yupo katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la nne mfululizo za Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga inayoongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 73 kupitia mechi 27, ikiizidi Simba yenye pointi 69 kupitia mechi 26, akiwa ameruhusu kufungwa mabao manane kati ya 10 ilizofungwa timu hiyo.