DB Lioness yatema ndoo WBDL, Srelio ikishuka daraja
Muktasari:
- DB Lioness ilitwaa taji la ubingwa huo mwaka jana, baada ya kuifunga JKT Stars katika fainali ya michezo 3-0.
BINGWA mtetezi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (WBDL), DB Lioness, ametema ubingwa baada ya kushindwa kutinga hatua ya robo fainali.
DB Lioness ilitwaa taji la ubingwa huo mwaka jana, baada ya kuifunga JKT Stars katika fainali ya michezo 3-0.
Akizungumzia kupoteza utetezi wa ubingwa huo, nyota wa timu hiyo, Sophia Ally, amesema wameshindwa kutokana na kukosa maandalizi ya kutosha kabla ya msimu kuanza.
Sophia ametaja maandalizi hayo kuwa ni pamoja na timu hiyo kushindwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya ligi hiyo na kwamba wanakwenda kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.
Wakati huohuo, timu za Chui, Srelio na Mchenga BC zimeshuka daraja baada ya kushika nafasi tatu za mwisho katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika hatua nyingine, Tausi Royals imeendelea kutisha katika mashindano hayo baada ya kumaliza mzunguko kwa ushindi wa pointi 74-67 dhidi ya timu ya Jeshi Stars. Nyota wa timu hiyo, Divine Irakoze, amesema haikuwa rahisi kwa timu yake kumaliza bila kupoteza mchezo wowote.
Kuhusiana na mchezo wao na Jeshi Stars, amesema ulikuwa miongoni mwa michezo yao migumu.
Licha ya ugumu huo, amesema walimaliza mzunguko huo bila kufungwa na timu yoyote, huku akiahidi kuwa wataingia katika hatua ya robo fainali mchujo (playoff) wakiwa na nguvu zaidi.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Maureen Sizya amesema baada ya kutopoteza michezo katika mzunguko, wataingia hatua ya playoff wakiwa na morali kubwa.
Kwa mujibu wa Maureen, hatua ya mchujo (playoff) itakuwa na ushindani mkubwa zaidi, hivyo Tausi Royals inatarajia kuongeza nguvu na maandalizi ili kukabiliana na changamoto za hatua hiyo. Ushindi wa timu hiyo umepatikana baada ya muda wa nyongeza wa dakika 5, kutokana na timu hizo kufungana pointi 62-62 katika robo zote nne.
Baada ya kuongezewa muda huo, Tausi Royals ilifunga pointi 12, huku Jeshi Stars ikifunga pointi tano. Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua ulifanyika katika Uwanja wa Don Bosco, Oyster Bay. Robo ya kwanza ilianza kwa mchezo huo huku timu hizo zikifungana pointi 13-13.
Katika robo ya pili Tausi Royals ilifunga pointi 24-19, 10-13, 15-17 na baada ya hapo dakika tano ziliongezwa ikafunga pointi 12 na Jeshi Stars ikifunga tano.
Kwenye mechi hiyo Anamary Cypian anayekipiga Jeshi Stars alifunga pointi 22 akifuatiwa na Witness Mapunda aliyetupia alama 17.
Kwa upande wa Tausi Royals, alikuwa Judith Pantaleo aliyefunga pointi 18, akifuatiwa na Tumaini Ndosi aliyefunga pia pointi 18, huku Divine Irakoze akifunga pointi 16. Timu ya Tausi Royals imemaliza mzunguko huo kwa pointi 32, ikifuatiwa na Reel Dream yenye pointi 30, JKT 30, DB Troncatti 28, Jeshi Stars 28, Vijana Queens 28, Ukonga Queens 26 na Polisi Stars 25.
Robo fainali itachezwa kati ya Tausi Royals dhidi ya Polisi Stars, Reel Dream dhidi ya Ukonga Queens, JKT Stars dhidi ya Vijana Queens na DB Troncatti dhidi ya Jeshi Stars. Hata hivyo, Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya BDL, Shabani Mahobonya, amesema ratiba ya hatua ya robo fainali itatangazwa hivi karibuni.