Dar City yazidi kuwa tishio BDL
Muktasari:
- Dar City imekuwa ikionyesha uwezo wa kubadili mifumo ya uchezaji mara kwa mara ndani ya mchezo, jambo linalowafanya wapinzani wake kushindwa kuendana na kasi yake.
DAR City imeendelea kuwa tishio katika Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), baada ya kuichapa Mlimani BC kwa pointi 81-45 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Don Bosco, Upanga.
Dar City imekuwa ikionyesha uwezo wa kubadili mifumo ya uchezaji mara kwa mara ndani ya mchezo, jambo linalowafanya wapinzani wake kushindwa kuendana na kasi yake.
Katika mchezo dhidi ya Mlimani BC, Dar City ilianza kwa utulivu katika robo ya kwanza huku ikiisoma timu hiyo na kutambua uwezo wake.
Hata hivyo, kuanzia dakika ya tano ya robo ya kwanza, Dar City ilibadili mfumo na kuanza kutumia presha (press) katika eneo la Mlimani BC, hali iliyowafanya wachezaji wa timu hiyo kushindwa kuutegua mfumo huo.
Katika mpira wa kikapu, presha ni mbinu ya ulinzi ambayo timu huweka shinikizo kwa mpinzani kwa kumfuata na kumkaba kwa karibu katika maeneo mbalimbali ya uwanja, badala ya kusubiri mpinzani afike katika eneo lao la ulinzi. Lengo lake ni kumlazimisha mpinzani kufanya makosa au kupoteza mpira.
Mlimani BC pia ilikumbwa na changamoto katika upigaji wa mipira ya pointi mbili. Timu hiyo ilipiga jumla ya mipira 37 ya pointi mbili, lakini ilifanikiwa kupata pointi kupitia mipira 14 pekee.
Wachezaji waliohusika katika mipira hiyo ni David Amisi, aliyepiga mipira minane na kufunga mitatu; Merva Bandu, aliyepiga mmoja na kukosa; Lukambali Daniel, aliyepiga mitatu na kukosa yote; John Thomas, aliyepiga minne na kufunga mmoja; na Adamu Michael, aliyepiga mitatu na kufunga mmoja.
Wengine ni Andrew Malando, aliyepiga mmoja na kukosa; Leancy Bukasa, aliyepiga 10 na kufunga saba; Enock Kakuba, aliyepiga minne na kufunga miwili; Shalom Ikendingwe, aliyepiga minne na kufunga miwili; na Shalom Mwakayosi, aliyepiga mitatu na kukosa yote. Dar City iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 24-10, 15-6, 22-13 na 20-16.
Jonas Mushi alikuwa mfungaji bora wa Dar City akiwa na pointi 20, akifuatiwa na Ally Abdallah aliyefunga pointi 15.
Kwa upande wa Mlimani BC, Jeancy Bukasa aliongoza kwa kufunga pointi 19, huku David Amisi akifunga pointi tisa.