Daktari Tausi atimkia Namungo
Muktasari:
- Hatua yake ya kujiunga na Namungo inaongeza orodha ya wanawake wanaopata nafasi za kufanya kazi katika soka la wanaume, akiwamo Fatma Omary, maarufu Fettyone, ambaye ni kocha wa makipa wa JKT Tanzania.
ALIYEWAHI kuwa mtaalamu wa tiba ya viungo wa Tausi FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake, Mary Gwatenda, amejiunga na Namungo FC ya Ligi Kuu Bara kwa upande wa wanaume kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Gwatenda, aliyeitumikia Tausi kwa msimu mmoja, sasa anaanza ukurasa mpya wa taaluma yake ndani ya kikosi hicho cha wanaume, akitumia uzoefu alioupata katika timu za wanawake na wanaume.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gwatenda amesema kufanya kazi na timu za wanaume si jambo geni kwake, akifichua kuwa tayari alipata uzoefu huo akiwa Alliance kabla ya kujiunga na Tausi FC.
“Kabla nilishafanya kazi na timu za Alliance, kwa hiyo kwangu tayari nina uzoefu na timu za kiume, lakini hakuna ugumu mkubwa kuwahudumia wanawake na wanaume,” amesema Gwatenda.
Kabla ya kujiunga na Tausi, Gwatenda alifanya kazi na timu za Alliance za wanawake na wanaume katika msimu wa 2024/2025, jambo lililompa uzoefu wa kuhudumia wachezaji wa jinsia zote.
Hatua yake ya kujiunga na Namungo inaongeza orodha ya wanawake wanaopata nafasi za kufanya kazi katika soka la wanaume, akiwamo Fatma Omary, maarufu Fettyone, ambaye ni kocha wa makipa wa JKT Tanzania.