Dakika 45 Bajaber, kocha atia neno
Muktasari:
- Bajaber Mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Januari 10,2026 alipocheza kwa dakika tisa tu kwenye mechi ya nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar, alipokaa chini mwenyewe huku akishika mguu wake wa kushoto nyuma ya paja.
MASHABIKI wa Simba wamemuona kiungo wao Mkenya Mohammed Bajaber ambaye dakika zake 45 zimewafurahisha huku kocha wake Steve Barker akielez hesabu zake kwa staa huyo.
Bajaber Mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Januari 10,2026 alipocheza kwa dakika tisa tu kwenye mechi ya nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar, alipokaa chini mwenyewe huku akishika mguu wake wa kushoto nyuma ya paja.
Kwenye mchezo huo ambao Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1, Bajaber alitolewa baadaye dakika ya 11 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa winga wa timu hiyo Kibu Denis,ukiwa pia mchezo wa kwanza wa kocha Steve Barker alopoanza kazi kwenye ligi.
Jana, Simba ikicheza dhidi ya Mafunzo kwenye mchezo wa robo fainali kiungo huyo alipewa dakika 45 za kipindi cha pili akiingia kuchukua nafasi ya winga kinda Ladack Chasambi akiingia sambamba na mfungaji wa bao hilo lililowapa ushindi wekundu hao Seleman Mwalimu.
Ndani ya dakika 45 Bajaber alionyesha ufundi safi akipiga pasi jumla 36 ambapo moja pekee ilipotea na zingine 35 zikifika sawasawa, akipiga pia krosi moja akitokea upande wa kushoto iliyomkosa mlengwa, akipokonya mpira mara moja.
Kiungo huyo aliyefunga bao moja mpaka sasa kwenye ligi kabla ya kuondolewa kwenye mfumo wa wachezaji wa msimu huu kutokana na majeraha, alionyesha pia kujaribu kupambana kwa nguvu katika matukio matatu na mawili kufanikiwa kuulinda mpira.
Bajaber hakufanya shambulizi la hatari sana kwenye mchezo huo lakini alionyesha kuimarika akianza kuondoa uwoga wa kuweza kuumia kama ambavyo alionekana akipata shida kwenye mechi za nyuma.
Baada ya mchezo huo kocha Barker amesemaamefurahia kumuona bajaber akirejea akisema ameonyesha uwezo mzuri uwanjani lakini bado anahitaji kuimarishwa taratibu.
Barker amesemaanatamani kuwa na kiungo huyo kwenye mechi za ligi ambapo kila anapokuwa uwanjani anaona timu pinzani zinamuogopa huku mashabiki wa Simba wakimfurahia kumuona.
“Ilikuwa nzuri kumuona Mohammed bajaber akirudi uwanjani baada ya majeraha tofauti ya muda mrefu, ni kiungo mshindani unaona dakika 45 tu amejaribu kuonyesha kile ambacho wengi tunatamani kukiona kwake,” amesema Barker.
“Nilitaka aje kwenye mechi hizi ili ziweze kumsaidia kumuimarisha, natamani sana kumuona ndani ya timu kama ambavyo unaona akiwa uwanjani anapoingia tu hata wapinzani wanamuogopa kwa kushtuka lakini mashabiki nao wanamfurahia sana.”