COREFA yageuka mbogo kwa timu Pwani
Muktasari:
- Mwenyekiti wa COREFA, Robert Munisi, amesema mkoa huo umejidhatiti kuhakikisha mpira unafundishwa na watu wanaokidhi vigezo.
CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), kimetoa amri kwa timu zote mkoani humo kuhakikisha zinakuwa na makocha rasmi na itakayokiuka haitoruhusiwa kushiriki mashindano yoyote ya soka katika mkoa huo.
Mwenyekiti wa COREFA, Robert Munisi, amesema mkoa huo umejidhatiti kuhakikisha mpira unafundishwa na watu wanaokidhi vigezo.
“Nitumie fursa hii kuwatangazia kuwa kuanzia sasa, timu yoyote ambayo haitokuwa na kocha angalau mwenye leseni D, haitoruhusiwa kushiriki mashindano ndani ya mkoa wa Pwani,” alisema Munisi.
Munisi aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa mashindano ya Meeting Point Super Cup yanayoshirikisha klabu nne kubwa za soka mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Mohammed Lacha, amezitaja timu hizo kuwa ni Barberian, Nyika, Nyumbu na Kiduli.
“Mimi na kamati yangu tumejipanga vizuri sana kuhakikisha mashindano haya yanaleta tija. Ukubwa wa mash indano haya mtauona kupitia zawadi na wageni ambao watashiriki,” alisema Lacha.
Mdhamini wa mashindano hayo, Luckyness Mokiwa, amewaomba mashabiki wa soka mkoani Pwani kujitokeza kwa wingi katika mechi hizo.
Mechi hizo zitachezwa kwa mtindo wa mtoano ambapo katika nusu fainali, Barberian itacheza na Nyumbu huku Nyika ikikabiliana na Kiduli.
Mechi za nusu fainali zitachezwa Septemba 12, 2026 na Fainali pamoja na mechi ya kuwania nafasi ya tatu zitachezwa Septemba 19, 2026.