Lukindo apata matumaini Namungo
Muktasari:
- Lukindo aliyewahi kuzichezea Mbao FC na KenGold, kwa sasa anakiwasha Namungo na amekuwa katika kiwango bora kikosini akijivunia bao moja na asisti mbili hadi sasa.
Pamoja na kukiri ugumu wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kiungo mshambuliaji wa Namungo, Herbert Lukindo amesema uhakika wa namba na kiwango binafsi vinampa matumaini ya kuipa matokeo mazuri timu hiyo.
Lukindo aliyewahi kuzichezea Mbao FC na KenGold, kwa sasa anakiwasha Namungo na amekuwa katika kiwango bora kikosini akijivunia bao moja na asisti mbili hadi sasa.
Namungo iliyowahi kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2020-2021 ikifika hadi hatua ya makundi, katika michezo sita iliyocheza Ligi Kuu Bara msimu huu imekusanya pointi sita sawa na wastani wa pointi moja kila mchezo na kuwa nafasi ya 11.
Lukindo alisema licha ya matokeo hayo kutokuwa mazuri sana, lakini ligi imekuwa ngumu na kila timu imejipanga kushinda akieleza kuwa hali hiyo inawapa presha kupambania pointi tatu kila mchezo ili kujiweka pazuri.
Kuhusu kiwango chake, nyota huyo amekiri msimu huu kuwa mzuri kwake na kuaminiwa na benchi la ufundi, akieleza kuwa majeraha ya msimu uliopita ndio yalimpa ugumu lakini kwa sasa yuko fiti na imara.
“Siyo matokeo mazuri kwa ujumla kwakuwa tumepoteza mechi tatu mfululizo tukiruhusu pia idadi kubwa ya mabao, lazima tujisahihishe tuweze kurejesha makali yetu na kuweka pazuri timu.
“Nashukuru msimu huu hali si mbaya na ni kutokana na uimara wa afya, msimu uliopita nilipitia magumu ila nimeimarika, kocha ameniamini ndio maana nafanya kazi kutimiza wajibu wangu,” alisema Lukindo.
Winga huyo aliongeza kuwa, kwa sasa akili na mawazo yao ni kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, akieleza kuwa licha ya ugumu wake, lakini wanahitaji kushinda ili kuondoa presha kikosini.
Namungo haina matokeo mazuri hadi sasa ikiwa imeshinda mechi mbili tu kati ya sita ilizocheza, ikipoteza michezo mitatu mfululizo ugenini dhidi ya JKT Tanzania (2-1), Singida Black Stars (3-2) na Azam (2-0). Kabla ya hapo, ilianza ligi kwa kichapo cha mabao 3-1 nyumbani dhidi ya Yanga. Mechi mbili ilizoshinda zote nyumbani dhidi ya Geita Gold (1-0) na Fountain Gate (1-0)