Clara Luvanga ana kibarua leo Marekani
Muktasari:
- Washington Spirit inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi yenye ushindani mkubwa duniani, ikiwa imejikusanyia pointi 46.
MSHAMBULIAJI Clara Luvanga leo ana kibarua Marekani, wakati klabu yake ya Washington Spirit ikiikabili Houston Dash katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake (NWSL) itakayopigwa kwenye Uwanja wa Audi Field.
Washington Spirit inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi yenye ushindani mkubwa duniani, ikiwa imejikusanyia pointi 46.
Katika mechi iliyopita dhidi ya Angel City FC, Clara alipata nafasi ya kuingia katika dakika ya 64 na kucheza dakika 26, ikiwa ni mechi yake ya kwanza tangu aliposajiliwa na miamba hiyo ya Marekani.
Hatua hiyo imekuwa mwanzo mzuri kwa nyota huyo wa Twiga Stars ambaye alijiunga na Washington Spirit kwa mkataba wa miaka minne akitokea klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Akiwa na Al-Nassr msimu uliopita, Clara alionyesha kiwango bora baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini Saudi Arabia akipachika jumla ya mabao 24.
Baada ya kucheza dakika hizo benchi la ufundi la timu hiyo linaweza kumwamini zaidi na kumpa nafasi au kuanza kikosini leo ili kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji.