Clara Luvanga aanza kukiwasha Marekani
Muktasari:
- Clara aliyeandika rekodi ya usajili wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake alipotokea Al Nassr ya Saudi Arabia na kutua Washington Spirit, amecheza mechi hiyo dhidi ya Angel City FC katika Ligi Kuu Wanawake Marekani akitokea benchi.
MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Clara Luvanga baada ya kutua Washington Spirit, leo Jumapili Septemba 27, 2026 amefanikiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Wanawake Marekani.
Clara aliyeandika rekodi ya usajili wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake alipotokea Al Nassr ya Saudi Arabia na kutua Washington Spirit, amecheza mechi hiyo dhidi ya Angel City FC katika Ligi Kuu Wanawake Marekani akitokea benchi.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa Washington Spirit kufungwa bao 1-0, Clara aliingia uwanjani dakika ya 66 kuchukua nafasi ya mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Rosemonde Kouassi, hatua iliyomfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kucheza katika ligi hiyo.
Mshambuliaji huyo alionyesha ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Washington Spirit na kufanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa langoni mwa wapinzani wao ingawa hazikuzaa bao.
Katika dakika 24 alizocheza, Clara aligusa mpira mara 14, alipiga mashuti mawili, shuti lake moja lilipita nje ya lango, huku lingine likizuiwa na mabeki wa Angel City.
Dakika 24 kwenye mechi yake ya kwanza ni ishara njema kwa Clara ambaye amekuwa na kiwango bora tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Mtanzania huyo ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Wanawake Saudi Arabia akiwa na kikosi cha Al Nassr alipofunga mabao 24, anaendelea kuweka historia kwa soka la wanawake Tanzania.
Uhamisho wa Clara kutoka Al Nassr kwenda Washington Spirit ulitajwa kuwa ni Euro 1.7 milioni (Sh5.2 bilioni) na kumfanya kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka la wanawake duniani.