Clara: Kila nifanyacho ni rekodi
Muktasari:
- Katika kinyang’anyiro hicho, aliwashinda Miljana Ivanovic wa Houston Dash, Lia Godfrey wa San Diego Wave FC na Brecken Mozingo wa Utah Royals FC, jambo linaloonyesha namna bao lake lilivyovutia mashabiki wa ligi hiyo.
MSHAMBULIAJI wa Washington Spirit, Clara Luvanga amesema kila anachokifanya kwenye ligi ya Wanawake ni rekodi kwake.
Mshambuliaji huyo ameanza vizuri kwenye ligi ya Marekani ikiwa ndiyo kwanza amesajiliwa akitokea Al Nassr W ya Saudia ambako alionyesha kiwango bora.
Akizungumza na Mwanaspoti, Clara amesema “Kwangu kila ninachokifanya hapa ni rekodi na najisikia fahari binafsi kuona nikiandika historia kila leo.”
Clara amesema furaha yake ni kubwa baada ya kuanza safari hiyo kwa mafanikio, lakini kwa sasa hana presha ya kujiwekea idadi maalumu ya mabao anayopaswa kufunga msimu huu, akisisitiza kipaumbele chake ni kujifunza na kuizoea ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
“Kwangu ni kitu kizuri kuanza msimu na bao kwenye ligi ngumu kama ya Marekani ambayo ina wachezaji wengi wazuri na wa kiwango cha juu. Msimu huu ni wa kujifunza na kuisoma ligi, hivyo sijaweka malengo ya kupachika mabao mangapi kwa sasa,” amesema Clara.
Hadi sasa Mtanzania huyo ameweka rekodi tatu, mojawapo ni usajili wake wa kihistoria kutoka Al Nassr ya Saudi Arabia kwenda Washington Spirit Septemba 9, 2026.
Ripoti za vyombo mbalimbali vya habari ziliweka thamani ya uhamisho huo katika Dola 2.3 milioni, sawa na takribani Sh 5.9 bilioni, kiasi kilichomfanya atajwe kuwa mmoja wa wanasoka wa kike waliosajiliwa kwa fedha nyingi zaidi duniani.
Rekodi ya pili ni kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mechi ya ligi hiyo ya wanawake Marekani, baada ya kuingia katika mchezo wa kwanza wa Washington Spirit dhidi ya Angel City FC Septemba 26, mwaka huu.
Clara alitokea benchi na kucheza dakika 24, timu hiyo ikipoteza kwa bao 1-0. Rekodi ya tatu ilikuwa katika mchezo wake wa pili dhidi ya Houston Dash, Oktoba 4 na aliingia kipindi cha pili dakika ya 66 na kucheza dakika 25 kabla ya kufunga bao la ushindi dakika ya 84.
Bao hilo liliipa Washington Spirit ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo huo wa ugenini, huku Clara akiweka historia nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika Ligi Kuu ya Wanawake Marekani.
Ubora wa bao hilo haukuishia kuipa pointi tatu timu hiyo kwani lilichaguliwa kuwa bao bora la wiki baada ya Clara kuwashinda washindani wake katika kura za mashabiki kupitia mitandao ya kijamii.
Katika kinyang’anyiro hicho, aliwashinda Miljana Ivanovic wa Houston Dash, Lia Godfrey wa San Diego Wave FC na Brecken Mozingo wa Utah Royals FC, jambo linaloonyesha namna bao lake lilivyovutia mashabiki wa ligi hiyo.