Clara Luvanga afungua ukurasa mpya wa mabao Marekani
Muktasari:
- Mchezo huo ulichezwa jana Jumapili, Oktoba 4, 2026 katika Uwanja wa Shell Energy Stadium, Houston, Texas, Marekani, ambapo Luvanga aliingia kipindi cha pili na kufunga bao la ushindi katika dakika ya 84.
Mshambuliaji wa Tanzania, Clara Luvanga, ameanza kuandika historia katika soka la wanawake Marekani baada ya kufunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ya Wanawake Marekani na kuisaidia Washington Spirit kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Houston Dash.
Mchezo huo ulichezwa jana Jumapili, Oktoba 4, 2026 katika Uwanja wa Shell Energy Stadium, Houston, Texas, Marekani, ambapo Luvanga aliingia kipindi cha pili na kufunga bao la ushindi katika dakika ya 84.
Luvanga alipokea pasi ya Claudia Martínez iliyomkuta akiingia kwenye eneo la hatari, kabla ya kutumia nafasi hiyo kuifungia Washington Spirit bao la tatu kwa shuti la mguu wa kulia lililodumu hadi mwisho wa mchezo.
Bao hilo ni hatua kubwa kwa Luvanga ambaye hivi karibuni aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kujiunga na ligi hiyo.
Mchezo huo ulikuwa wa pili kwa Luvanga tangu asajiliwe na Washington Spirit Septemba 9, 2026, akitokea Al Nassr ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka minne.
Katika mchezo wake wa kwanza, aliingia akitokea benchi dhidi ya Angel City FC Septemba 26, 2026 ambapo Washington Spirit ilifungwa bao 1-0.
Mchezo wa Houston ulimpa Luvanga nafasi ya pili ya kuonekana uwanjani, na safari hii akatumia dakika hizo kuandika jina lake kwenye historia ya soka la wanawake Tanzania.
Washington Spirit ilianza mchezo huo kwa kupata bao kupitia Tara Rudd katika dakika ya 11, kisha Houston kusawazisha kupitia Miljana Ivanović katika dakika ya 44.
Sofia Cantore aliirudisha Washington Spirit uongozini katika dakika ya 51, lakini Ivanović alisawazisha tena ktika dakika ya 59.
Luvanga ndiye aliyevunja sare hiyo dakika ya 84, akiipa Washington Spirit ushindi na pointi tatu muhimu.
Kwa Luvanga, bao hilo linaanza kumuweka katika nafasi nzuri ya kujaribu kurudia historia ya msimu uliopita ambao aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia baada ya kupachika mabao 24.