Clara Luvanga aipeleka Washington Spirit fainali NWSL
Muktasari:
- Luvanga aliyejiunga na Washington Spirit Septemba mwaka huu, alifunga bao hilo dakika ya 56 baada ya kutumia makosa ya safu ya ulinzi ya Utah Royals, ambapo beki Nuria Rábano alicheza pasi dhaifu ya kurudi nyuma iliyomnufaisha mshambuliaji huyo na kuandika bao la ushindi.
WASHINGTON, MAREKANI: MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Clara Luvanga, ameendelea kung'ara katika Ligi ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL) baada ya kufunga bao la ushindi lililoipa Washington Spirit ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Utah Royals na kufuzu fainali ya mashindano hayo.
Luvanga aliyejiunga na Washington Spirit Septemba mwaka huu, alifunga bao hilo dakika ya 56 baada ya kutumia makosa ya safu ya ulinzi ya Utah Royals, ambapo beki Nuria Rábano alicheza pasi dhaifu ya kurudi nyuma iliyomnufaisha mshambuliaji huyo na kuandika bao la ushindi.
Bao hilo linamfanya Luvanga kufikisha manne katika mechi saba alizocheza za Ligi Kuu Wanawake Marekani, ambapo jumla amehusika kwenye mabao saba baada ya kuasisti matatu.
Katika mchezo huo wa leo Jumamosi Novemba 14, 2026 uliochezwa Audi Field uliopo mji wa Washington DC, Utah Royals ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya pili kupitia Cloé Lacasse aliyefunga kwa mpira wa kona uliokwenda moja kwa moja wavuni, bao lililowekwa kwenye rekodi ya kuwa la haraka zaidi katika historia ya mechi za mtoano za NWSL, likifungwa baada ya dakika moja na sekunde 57.
Washington Spirit ambayo ilikuwa mwenyeji, ilisawazisha dakika ya nane kupitia Sofia Cantore aliyemalizia pasi ya Trinity Rodman, kabla ya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1. Katika kipindi cha pili, Luvanga aliibuka shujaa kwa bao lake lililohakikisha timu hiyo inasonga mbele.
Ushindi huo umeiwezesha Washington Spirit kucheza fainali ya NWSL kwa mara ya tatu mfululizo, ikiwa ni klabu ya pili katika historia ya ligi hiyo kufikia hatua hiyo baada ya North Carolina Courage kufanya hivyo kati ya mwaka 2017 na 2019.
Fainali hiyo itachezwa Audi Field, Novemba 21, 2026, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Spirit kucheza mchezo wa kuwania ubingwa mbele ya mashabiki wake nyumbani.
Timu hiyo sasa inasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Gotham FC na Kansas City Current.