Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Clara Luvanga hakamatiki Marekani

Muktasari:

  • Katika mchezo huo, Clara aliingia akitokea benchi na kutengeneza bao la pili lililofungwa na Trinity Rodman dakika ya 85, baada ya Spirit kupata bao la kwanza dakika ya 62 baada ya Michelle Alozie kujifunga.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga ameendelea kuonyesha kiwango bora akiwa na klabu yake ya Washington Spirit, baada ya kuchangia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chicago Stars FC, katika mchezo wa Ligi ya Wanawake ya Marekani (NWSL), uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Audi Field, Washington DC.

Katika mchezo huo, Clara aliingia akitokea benchi na kutengeneza bao la pili lililofungwa na Trinity Rodman dakika ya 85, baada ya Spirit kupata bao la kwanza dakika ya 62 baada ya Michelle Alozie kujifunga.

Pasi hiyo aliyoitoa imeongeza thamani ya mchango wake kwa timu hiyo.

Mafanikio makubwa yaliyomweka Clara katika vitabu vya historia ya soka la Tanzania, ni bao lake alilofunga Oktoba 5, 2026 dhidi ya Houston Dash.

Alifunga bao la ushindi dakika ya 84 na kuisaidia Spirit kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Bao hilo lilikuwa la kihistoria kwa kuwa lilimfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika NWSL, mafanikio yanayoonyesha hatua kubwa aliyopiga katika safari yake ya soka nje ya Tanzania.

Tangu ajiunge na Washington Spirit, Clara amecheza jumla ya dakika 235, akifunga mabao mawili na kutoa pasi moja iliyozalisha bao. Amekuwa na wastani wa alama 6.8 kwa kila mchezo, takwimu zinazoonyesha mchango wake licha ya kutopata muda mwingi wa kucheza.

Makali yake yameonekana pia katika michezo ya hivi karibuni, na alifunga bao dhidi ya Kansas City Current Oktoba 25. Alicheza dakika 79 dhidi ya Gotham FC Oktoba 17.

Ushindi dhidi ya Chicago Stars umeifanya Spirit kuhitimisha msimu wa kawaida ikiwa na ushindi 15, sare nane na vipigo vinne, matokeo yaliyoiwezesha kufuzu hatua ya mtoano na kuendelea kuwania ubingwa.

Mkurugenzi wa Michezo wa Washington Spirit, James Hocken ameonyesha kuvutiwa na uwezo wa Clara, akieleza mshambuliaji huyo Mtanzania anaongeza nguvu mpya katika safu ya ushambuliaji kuelekea hatua ya mtoano.

“Clara anaongeza kitu katika safu yetu ya ushambuliaji tunapoelekea hatua ya mtoano. Licha ya umri wake mdogo, ameonyesha uwezo wa kufunga mabao kwa njia tofauti, ni matarajio yangu ataendelea kufanya vizuri katika ligi hii,” alisema Hocken. Kauli hiyo inaonyesha imani ya uongozi wa Spirit kwa uwezo wa Clara, ambaye licha ya umri wake mdogo wa miaka 21, ameanza kuonyesha dalili za kuwa mchezaji muhimu.

Pia ni ishara kuwa klabu ina matarajio makubwa juu ya maendeleo yake katika ligi yenye ushindani mkubwa.

Sasa macho ya mashabiki yataelekezwa kwenye mchezo wa hatua ya mtoano dhidi ya Portland Thorns unaotarajiwa kupigwa Novemba 8, 2026.

Huo ni mchezo muhimu katika kuwania nafasi ya kucheza fainali, huku Clara akitarajiwa kuwa sehemu ya mipango ya kikosi.