Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Clara akosa ubingwa Marekani

CLARA Pict

Muktasari:

  • Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Clara aliendelea kuaminiwa na benchi la ufundi la Washington Spirit, akicheza dakika 74 kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Rosemonde Kouassi.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga ameshindwa kuisaidia timu yake ya Washington Spirit kutwaa ubingwa wa Ligi ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL) 2026 baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Kansas City katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Audi Field, nyumbani kwa Spirit.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Clara aliendelea kuaminiwa na benchi la ufundi la Washington Spirit, akicheza dakika 74 kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Rosemonde Kouassi.

Dakika hizo 74 zinaendelea kuwa sehemu ya safari ya mshambuliaji huyo tangu alipojiunga na Washington Spirit akitokea Al Nassr ya Saudi Arabia, Septemba 2026.

CLA 01

Katika mchezo huo wa fainali, Clara alijitahidi kuisaidia Spirit kupata bao la kuongoza, lakini alikumbana na safu imara ya ulinzi ya Kansas City.

Dakika ya 41, alianzisha shambulizi la haraka na kupeleka mpira ndani ya eneo la hatari akimtafuta Sofia Cantore, ambaye alijaribu kupiga shuti lakini lilizuiwa na mabeki wa Kansas City.

Dakika tatu baadaye, Clara alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Temwa Chawinga.

CLA 02

Kipindi cha pili aliendelea kuwa sehemu muhimu ya mashambulizi ya Washington, akipata nafasi ya kupiga shuti dakika ya 58, lakini mpira ulimgonga beki Kayla Sharples usoni na kuzuia hatari iliyokuwa ikielekea langoni mwa Kansas City.

Dakika ya 61, alishirikiana na Trinity Rodman kuanzisha shambulizi lililomfikisha Leicy Santos karibu na lango, hata hivyo shuti la kiungo huyo lilitoka nje.

Clara aliendelea kutafuta bao, lakini dakika ya 72 alikosa nafasi nyingine baada ya Rodman kumpa pasi nje kidogo ya eneo la hatari. Shuti lake lilipaa pembeni mwa lango kabla ya kutolewa uwanjani dakika mbili baadaye.

Kansas City ilitangulia kupata bao dakika ya 54 kupitia Vanessa DiBernardo, aliyefunga moja kwa moja kwa mpira wa kona. Debinha ameongeza bao la pili katika dakika za nyongeza, kabla ya Trinity Rodman kuifungia Washington Spirit bao la kufutia machozi.

CLA 03

Ushindi huo uliipa Kansas City ubingwa wa NWSL 2026, huku Washington Spirit ikikosa nafasi ya kutwaa taji hilo mbele ya mashabiki wake.

Clara, mwenye umri wa miaka 21, alijiunga na Washington Spirit Septemba 2026 kwa mkataba wa miaka minne unaotarajiwa kumuweka klabuni hapo hadi mwaka 2029.

Mshambuliaji huyo alitua Marekani akiwa na rekodi nzuri baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Wanawake Saudi Arabia, ambako alifunga mabao 24 katika mechi 14 akiwa na Al Nassr na kutwaa tuzo ya mfungaji bora.