Chukwu avuta Sh1.8 bilioni arabuni
Muktasari:
- Chukwu ambaye alikuwa akihusishwa kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ametimkia Lebanon huku chanzo cha karibu na mchezaji huyo kikieleza kuwa amevuta Sh1.8 bilioni kama pesa ya usajili baada ya kusajiliwa akiwa mchezaji huru.
KIUNGO wa zamani wa Singida Black Stars, Morice Chukwu, amejiunga na Jwaya SC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Lebanon kwa mkataba wa miaka miwili, uhamisho unaotajwa kuwa amepiga pesa ndefu.
Chukwu ambaye alikuwa akihusishwa kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ametimkia Lebanon huku chanzo cha karibu na mchezaji huyo kikieleza kuwa amevuta Sh1.8 bilioni kama pesa ya usajili baada ya kusajiliwa akiwa mchezaji huru.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, Chukwu atakuwa akilipwa mshahara wa Sh90 milioni kila mwezi. Kwa hesabu za mwaka mmoja pekee, mshahara huo unafikisha Sh1.08 bilioni, huku kwa mkataba wake wa miaka miwili mshahara ukifikia Sh2.16 bilioni.
“Chukwu alikuwa na chaguo kadhaa baada ya kumaliza mkataba wake na Singida Black Stars, lakini amefikia makubaliano ya kujiunga na Jwaya SC ambao walikuja na ofa kubwa, hivyo akaamua aende Lebanon na tunaamini kwa alichokifanya Singida anaweza kuwa msaada huko,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.
“Yanga ilimtafuta kuangalia uwezekano wa kumpata lakini hawakumrudia mara ya pili, kwahiyo alikuwa na machaguo ni sehemu ipi aweze kwenda, ndipo akachagua Lebanon.”
Dili hilo limekuja baada ya Chukwu kumaliza mkataba wake na Singida Black Stars mwisho wa msimu wa 2025-2026, hali iliyompa uhuru wa kuamua mwenyewe klabu atakayojiunga nayo baada ya kuwa na msimu bora.
Msimu wa 2025-2026, Chukwu alicheza mechi 17 za Ligi Kuu Bara akiwa na Singida Black Stars kati ya 30 na kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hiyo iliishia hatua ya makundi, kiungo huyo alitumika mechi tano.
Kiungo huyo mkabaji mwenye umri wa miaka 24, alikamilisha uhamisho wake huo Agosti 15, 2026. Chukwu anatumia mguu wa kulia na amejenga historia yake ya soka katika klabu mbalimbali nchini Nigeria na Tanzania.
Chukwu amecheza mechi 147 katika Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL), akifunga mabao sita na kutoa pasi sita za mabao. Pia ameshiriki mashindano ya klabu Afrika, akiwa na mechi 22 za Kombe la Shirikisho la CAF na sita za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika rekodi yake ya mashindano ya Afrika, Chukwu amefunga bao moja katika Kombe la Shirikisho la CAF na kutoa asisti moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Pia amecheza mechi tano za mchujo wa NPFL, akifunga bao moja.
Chukwu anajiunga na Jwaya akiwa na mataji mawili ya Ligi Kuu ya Nigeria kwenye historia yake. Alitwaa ubingwa akiwa na Akwa United msimu wa 2020-2021, kabla ya kusaidia Rivers United kutwaa taji hilo msimu wa 2021-2022.
Kiungo huyo alianza kucheza soka la ngazi ya juu akiwa na Go Round FC, kabla ya kujiunga na Akwa United Septemba 2019. Alijiunga na Rivers United Mei 2021, kisha akahamia Fountain Gate Julai 2023.
Katika msimu wa 2023-2024, Chukwu alijiunga na Ihefu SC ambayo sasa inafahamika kwa jina la Singida Black Stars. Baadaye alitumia sehemu ya msimu wa 2024-2025 kwa mkopo katika kikosi cha TRA United, kabla ya kurejea Singida baada ya kumalizika kwa kipindi hicho cha mkopo.
Jwaya imekuwa klabu ya hivi karibuni katika safari ya Chukwu, huku sasa akianza ukurasa mpya katika Ligi Kuu ya Lebanon. Ujio wake usajili wake unamuongeza uzoefu katika safari yake ya soka.