Christopher: Dabi ya Kariakoo haitakuwa nyepesi
Muktasari:
- Christopher amesema uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni katika vikosi vya timu hizo umeongeza ushindani wa nafasi, huku ukifanya mchezo huo kuwa mgumu kutabirika na hivyo matokeo yake hayawezi kuamuliwa kwa kuangalia ubora wa vikosi pekee.
KIUNGO wa zamani wa Simba, Edward Christopher, amesema mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa leo, Agosti 12, 2026, hautakuwa rahisi kutokana na ushindani na mvuto mkubwa wa Dabi ya Kariakoo.
Christopher amesema uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni katika vikosi vya timu hizo umeongeza ushindani wa nafasi, huku ukifanya mchezo huo kuwa mgumu kutabirika na hivyo matokeo yake hayawezi kuamuliwa kwa kuangalia ubora wa vikosi pekee.
“Kwa mechi ya Simba na Yanga haiwezi kuwa nyepesi. Hata kama Simba ikiwa na kikosi kidogo, bado Dabi ya Kariakoo itakuwa ngumu,” amesema Christopher.
Akizungumzia usajili wa Simba, Christopher alisema wachezaji waliosajiliwa wana uwezo mzuri, lakini jambo la msingi ni kuona namna watakavyoweza kuendana na kasi na ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Kulingana na ripoti ya kocha, nadhani imepelekea kuona upungufu katika nafasi husika. Wachezaji wote ni wazuri, labda kinachobaki ni kuona namna watakavyoendana na spidi ya ligi,” amesema.
Christopher, maarufu kama Eddo Boy, aliwahi kuichezea Simba B msimu wa 2012 na kuwa na msimu bora baada ya kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Super 8, huku yeye akiwa kinara wa mabao akiwa amefunga manane.
Uwezo wake ulimfanya apandishwe kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, kabla ya kuendelea na safari yake ya soka katika klabu mbalimbali.
Baadhi ya timu alizowahi kuichezea ni Polisi Morogoro msimu wa 2014/15, Toto African (2015/16), Kagera Sugar (2016-2018), Ruvu Shooting (2019/20) na Coastal Union msimu wa 2020/21.