Chasambi afichua jipya Singida
Muktasari:
- Chasambi ambaye ametua Singida BS akitokea Simba, amesema aliona mradi wa klabu hiyo na malengo yake ya kushiriki michuano ya kimataifa kama fursa muhimu ya kuendeleza kazi yake ya soka.
KIUNGO mpya wa Singida Black Stars, Ladack Chasambi, amefichua kuwa uwepo wa changamoto za kimataifa ndio miongoni mwa sababu kubwa zilizomvutia kujiunga na klabu hiyo, akiamini anaweza kupata nafasi ya kujipima katika kiwango cha juu zaidi.
Chasambi ambaye ametua Singida BS akitokea Simba, amesema aliona mradi wa klabu hiyo na malengo yake ya kushiriki michuano ya kimataifa kama fursa muhimu ya kuendeleza kazi yake ya soka.
Kiungo huyo baada ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza Simba, anaamini ndani ya Singida atapambana kuonyesha uwezo wake.
Singida Black Stars msimu ujao itawakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo, huku ikiwa nchini Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya kwa kushiriki Kombe la CECAFA Kagame.
“Moja ya vitu vilivyonivutia kuja Singida ni kuona timu ina malengo makubwa, hasa kushiriki mashindano ya kimataifa, hii ni nafasi nzuri kwangu kama mchezaji kuonyesha uwezo wangu na kusaidia timu kufikia malengo yake,” alisema Chasambi.
Mchezaji huyo alisema anafahamu ushindani utakuwa mkubwa kutokana na ratiba ya mashindano ambayo Singida itakutana nayo, lakini anaamini maandalizi mazuri na mshikamano wa wachezaji yanaweza kuifanya timu hiyo kufanya vizuri.
“Nimeona kikosi kina wachezaji wengi wazuri na viongozi wana malengo makubwa. Kazi yetu ni kufanya mazoezi kwa bidii, kusikiliza maelekezo ya kocha na kuhakikisha tunakuwa timu yenye ushindani,” alisema.
Chasambi ambaye amepata fursa ya kucheza mashindano ya CECAFA Kagame, alisema anatamani kuwa sehemu ya kikosi kitakachosaidia Singida kutetea taji hilo.