Carlinhos sasa rasmi

SASA ni rasmi mshambuliaji wa Yanga, Carlos Carlinhos ameruhusiwa kuanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake mapema wiki ijayo baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya paja. Daktari wa Yanga amesema alikuwa na matatizo mawili.

Lakini mshambuliaji mwenye nguvu na kasi, Yacouba Sogne aliumia nyama za paja katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na zilimfanya kukosa mchezo wa fainali dhidi ya Simba, na kuwa nje ya uwanja mpaka wakati huu kwa kushindwa kufanya mazoezi binafsi.

Daktari wa Yanga, Sheikh Mngazija alisema Carlinhos alikuwa na ratiba ya kufanya mazoezi binafsi ya nguvu pamoja na kuchezea mpira muda mrefu.

“Baada ya kupata matibabu hayo ya nyama za paja pamoja na uvimbe huo ambao alikuwa nao katika paja la kulia, kwa sasa tumemuangalia anaendelea vizuri na yale maumivu yote ya awali yameondoka na kilichobakia kwetu siku ambayo tutaanza mazoezi tutakuwa naye pamoja,” alisema.

“Carlihos alikuwa akiumwa vitu viwili kwa wakati mmoja hizo nyama za nyuma ya paja na uvimbe ulioota kwa mbele ya paja hilo la kulia, ameanza mazoezi mepesi.

“(Kuhusu Yacouba) tunampeleka tena hospitali ili kumfanyia vipimo vingine zaidi ili kufahamu shida ambayo inamsumbua ni ipi na kwa nini ameshindwa kupona katika matibabu ya awali na baada ya hapo ndio ataanza tiba mpya na kufahamu atakuwa nje ya muda gani.”