Bwenzi afichua siri ya kuifunga Simba
Muktasari:
- Bwenzi alifunga bao hilo dakika ya 63, wakati Mashujaa ikikubali kichapo cha mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Oktoba 13, 2026, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa FC, Selemani Rashid ‘Bwenzi’, amefichua siri ya bao la umbali mrefu alilofunga dhidi ya Simba, akisema alitumia nafasi ya kumwona kipa Mahamadou Kassali akiwa mbali na lango lake.
Bwenzi alifunga bao hilo dakika ya 63, wakati Mashujaa ikikubali kichapo cha mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Oktoba 13, 2026, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Simba ilipata mabao yake kupitia Libasse Gueye, Anicet Oura, Morice Abraham na Ismael Toure, kila mmoja akifunga bao moja, huku Elie Mpanzu akifunga mawili.
Bwenzi amesema alimwona Kassali akiwa mbele ya lango lake wakati akipokea pasi, ndipo akaamua kupiga shuti kali kutoka katikati ya uwanja.
Amesema bao hilo halikuwa la bahati pekee, kwani amekuwa akifanyia kazi mashuti ya mbali katika mazoezi, ingawa si kila jaribio lake huishia wavuni.
“Mazoezini huwa najaribu mara kwa mara kupiga mashuti ya mbali. Si kila ninalopiga huwa bao, lakini naona kwa kiwango kikubwa kile ninachokifanya mazoezini kinaanza kunilipa. Ni bahati mbaya tu tumepoteza mechi,” amesema Bwenzi.
Kiungo huyo amesema kufunga bao hilo licha ya timu yake kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao kumempa morali ya kuendelea kuonyesha kiwango kizuri, hasa baada ya kukaa muda mrefu bila kufunga bao katika Ligi Kuu.
Bao hilo limekuwa na kumbukumbu ya pekee kwa Bwenzi, kwani pia aliwahi kufunga katika mchezo ambao KenGold FC ya Mbeya ilipoteza kwa mabao 6-1 dhidi ya wapinzani wake Februari 5, 2025, wakati timu hiyo ikishiriki Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja.
Bwenzi alijiunga na Mashujaa FC Julai 19, 2025, akitokea KenGold. Kabla ya hapo, bao lake la mwisho katika Ligi Kuu lilikuwa lile alilofunga Februari 27, 2025, wakati KenGold ilipotoka sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, mshambuliaji Edward Songo aliifungia JKT Tanzania kwa penalti dakika ya 45+6, kabla ya Bwenzi kusawazisha dakika ya 85.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, bao lake dhidi ya Simba limehitimisha ukame wa siku 593 bila kufunga katika Ligi Kuu, sawa na mwaka mmoja, miezi saba na siku 16.