Burundi yatinga nusu fainali CECAFA U-20
Muktasari:
- Ushindi huo umeifanya Burundi kufikisha pointi sita baada ya kushinda michezo yake yote miwili na kuongoza Kundi C, huku mshambuliaji Amini Nshimirimana akiendelea kung’ara baada ya kufunga mabao yote mawili.
BURUNDI imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya kuwania tiketi ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (AFCON U20) kwa ukanda wa CECAFA, baada ya kuichapa Kenya mabao 2-0.
Ushindi huo umeifanya Burundi kufikisha pointi sita baada ya kushinda michezo yake yote miwili na kuongoza Kundi C, huku mshambuliaji Amini Nshimirimana akiendelea kung’ara baada ya kufunga mabao yote mawili.
Nshimirimana sasa amefikisha mabao manne katika michuano hiyo na kuwa kinara wa wafungaji, baada ya pia kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Sudan Kusini.
Katika michezo mingine ya siku hiyo, Rwanda na Ethiopia zilitoka suluhu katika Kundi A, wakati Sudan iliichapa Djibouti mabao 3-0 katika Kundi C. Kenya sasa italazimika kuelekeza nguvu katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi C dhidi ya Sudan Kusini, ikitafuta nafasi ya kumaliza ikiwa timu bora ya pili kati ya makundi yote matatu. Michuano hiyo inayoshirikisha timu tisa imegawanywa katika makundi matatu yenye timu tatu kila moja. Vinara wa kila kundi watafuzu moja kwa moja nusu fainali, huku timu yenye nafasi ya pili iliyo na matokeo bora zaidi ikikamilisha idadi ya timu nne za hatua hiyo.
Timu mbili zitakazofika fainali ndizo zitakayopata tiketi za kuiwakilisha CECAFA katika fainali za AFCON U20. Hatua ya makundi itafungwa kesho, Jumamosi, ambapo wenyeji Tanzania watacheza dhidi ya Ethiopia katika Kundi A, Kenya itakutana na Sudan Kusini, huku Sudan ikipambana na Uganda.