Ngorongoro Heroes kuivaa Ethiopia
Muktasari:
- Mchezo huo utapigwa saa 2:00 usiku, huku Tanzania ikiwa na nafasi ya kuwania pointi tatu na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
TIMU ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, kesho Jumamosi itarejea Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kukabiliana na Ethiopia katika mchezo wa pili wa Kundi A kuwania kufuzu Fainali za AFCON U-20.
Mchezo huo utapigwa saa 2:00 usiku, huku Tanzania ikiwa na nafasi ya kuwania pointi tatu na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
Tanzania ilianza mashindano hayo kwa kishindo Septemba 15, ikiichapa Rwanda mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Kundi A. Ushindi huo uliifanya Ngorongoro Heroes kuanza kampeni ikiwa na pointi tatu, mabao matatu ya kufunga na bila kuruhusu bao. Matokeo hayo pia yameweka presha kwa Ethiopia, ambayo sasa inahitaji matokeo mazuri ili kuendelea kuwa na nafasi ya kusonga mbele.
Kikosi cha kocha Mario Rivera Campesino kitaingia kwenye mchezo huo kikiwa na kumbukumbu ya kiwango kilichoonyesha dhidi ya Rwanda, hasa uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga.
Kocha huyo amesema timu hiyo ilianza vizuri kwa kupata ushindi na kwamba ingeweza kushinda kwa tofauti kubwa zaidi katika michezo mingine kutokana na nafasi nyingi wanazotengeneza.
Hilo linaifanya mechi dhidi ya Ethiopia kuwa mtihani mwingine wa namna vijana hao watakavyotumia nafasi wanazopata. “Maandalizi yanaendelea vizuri na tunakwenda kwenye mchezo huu tukiwa na ushindi wa kwanza, lakini tunatakiwa kuboresha matumizi ya nafasi kwa sababu tunaendelea kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Tukizitumia vizuri, tunaweza kupata ushindi wa mabao mengi katika michezo inayofuata,” amesema Campesino.
Mbali na mechi ya Tanzania, zitapigwa mechi nyingine mbili. Djibouti itakutana na Sudan saa 10:00 jioni, kabla ya mchezo mwingine wa siku hiyo kuwakutanisha Burundi na Kenya. Ratiba hiyo inaonyesha ushindani mkubwa unaotarajiwa katika michuano hiyo, huku kila taifa likisaka nafasi ya kufika hatua ya mwisho ya michuano hiyo ya vijana.