Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Buku tu, zinatosha kuzipa viwanja

Yusuf Manji, Mwenyekiti klabu ya Yanga (kushoto), Rais wa Simba, Evans Aveva (kulia).

Muktasari:

Pamoja na hali hiyo, nimelazimika kwa msaada wa binti yangu kuandika makala haya ikiwa ni zawadi ya Mwaka Mpya kwa wanamichezo wote nchini, hususan mashabiki wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga za Kariakoo Dar es Salaam.

KWA miaka miwili sasa, nimekua nasumbuliwa na ugonjwa baada ya kupata maradhi ya kiharusi Januari, 2014. Hadi sasa naendelea kuvumilia kwa vile kuugua ni mtihani wa Mwenyezi Mungu.

Pamoja na hali hiyo, nimelazimika kwa msaada wa binti yangu kuandika makala haya ikiwa ni zawadi ya Mwaka Mpya kwa wanamichezo wote nchini, hususan mashabiki wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga za Kariakoo Dar es Salaam.

Naziita klabu kongwe kwa vile zinaingia umri wa miaka 80, lakini bado hazijawa na miundombinu ya klabu za kisasa na kupata hadhi ya kuweza kuitwa klabu kubwa. Kwa hiyo zinahitaji kazi kubwa na ya ziada kuweza kufikia hadhi ya kuwa klabu kubwa.

Hivi sasa klabu hizo mbili zenye utani wa jadi zinazidiwa kwa hadhi na klabu changa ya Azam ya Dar es Salaam ambayo haijafikia hata miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Sizilaumu Simba na Yanga kwa hali walionayo kwani kama Azam isingemilikiwa na tajiri nayo ingekua imejifia au iko taabani kama zilivyo Pan African na Nyota Nyekundu za Dar es Salaam.

Pamoja na kwamba Simba na Yanga ziko katika hali hiyo ya kukosa hata viwanja vyake binafsi vya kufanyia mazoezi siyo kwamba sielewi Yanga inakiota chake cha Kaunda pale makao makuu yao, Jangwani, ila bado inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterani.

Simba nayo ina msitu wake kule Bunju pembezoni kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na wanachama wa klabu hiyo waliwahi kufanya usafi siku za nyuma, lakini wameutupa na hawajauendeleza na nimeuona siku za karibuni kupitia runinga hauko katika hali nzuri.

Klabu hizo kongwe hazipaswi kuwa katika hali hii kwa vile zina mashabiki mamilioni katika kila kona ya Tanzania na hata katika nchi za Afrika Mashariki, pia zina mashabiki waliotapakaa sehemu mbali mbali duniani.

Nakumbuka miaka ya 70 wakati nasoma Shule ya Msingi ya Wingwi iliyopo Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati tukienda kwenye michezo tulikuwa tunajigawa kwa itikadi ya ushabiki wa Simba na Yanga.

Nakumbuka vizuri nilikuwa nahodha wa ile klabu ambayo siku hizi imepewa jina la Wekundu Wa Msimbazi na Mdogo wangu Ambae ni Katibu wa tawi la Yanga Buguruni, Salim akivaa kitambaa cha unahodha kwa upande wa Kandambili.

Kwa maana hiyo, kama huko Pemba kuna mashabiki wa namna hiyo wa Simba na Yanga ni dhahiri na haina shaka kuwa klabu hizo ziko kwenye mioyo ya kila Mtanzania anayeishi upande wa Bara ambapo klabu hizo zinatoka. Kwa miaka mingi, Simba na Yanga zimekuwa zikiendeshwa kwa kutegemea wafadhili ambao wanatoa fedha zao mfukoni na kuzihudumia timu za soka za klabu hizo kuanzia usajili wa wachezaji hadi masuala ya kuendesha timu.

Wako wafadhili ambao waliwahi au wanaendelea kuzisaidia klabu hizo kimya kimya na wengine wakajitangaza kiasi cha kuwa kama viongozi kama ilivyotokea miaka ya karibuni kwa Azim Dewji wa Simba na Abbas Gulamali wa Yanga.

Wakati huo Simba ikiitwa Taifa kubwa na Yanga ikiitwa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, sasa Simba na Yanga zimepiga hatua kubwa zaidi kwani mbali na kutegemea wafadhili sasa zimeingia katika uendeshaji mpya wa timu wa kuwa na wadhamini. Zote zinadhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro na zinapata mgao kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Vodacom na Azam TV.

Uongozi wa Simba ulio chini ya Rais Evans Aveva na Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Yusuf Manji wakijipanga vyema na kuratibu vizuri kwa kuwatumia mamilioni ya mashabiki wao nchi nzima zinaweza kujipatia fedha nyingi ukawa mtaji wa kuziendeleza klabu hizo na kuapata maendeleo makubwa.

Kila moja kati ya klabu hizi haikosi mashabiki milioni 10 nchi nzima ambao kama watahamasishwa vizuri na kuwa tayari na kujengewa msingi wa kuamini kwamba fedha zao hazitapotea watakuwa tayari kwa kila mmoja kuchangia Sh1,000 kwa maendeleo ya klabu yake.

Kwa maendeleo ya sasa ukusanyaji wa fedha hizo unaweza kuwa rahisi kwa kufungua akaunti ya benki kwa ajili ya mashabiki ambao wako tayari kujitolea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuzichangia klabu hizo.

Wale ambao watachangia Sh 1,000 wanaweza wakatoa michango yao kwa kutumia mitandao ya simu za mikononi.

Iwapo yatakuwepo mafanikio kwa mashabiki au wapenzi milioni 10 kwa kila klabu kuchangia kila moja itapata kiasi cha Sh. 10 bilioni. Lakini hata kama walichangia wapenzi milioni moja tu ambayo ndiyo idadi ya chini kabisa kila klabu itajipatia Sh1 bilioni ambazo si fedha haba.

Hata hivyo, inaweza kuachana na utaratibu huo na ikaingia katika utaratibu wa kisasa zaidi kwa kuuza hisa jambo ambalo litamvutia kila Mtanzania ambaye hakuna asiye na hamu na shauku ya kuzimiliki klabu hizo kongwe na maarufu nchini.

Iwapo kila klabu itauza hisa milioni 10 kwa Sh1000 kila moja itapata Sh10 bilioni, ambazo inaweza kuekeza kwenye kampuni mbalimbali na kujengea viwanja angalau vya mazoezi.

Wapenzi hao watakuwa tofauti na walionunua hisa kwenye kampuni kwani wao hawatatarajia gawio la fedha, bali watakachotaka ni ushindi kwa timu zao.

Zikiwa na fedha klabu hizo zitakuwa na uwezo wa kuwasajili wachezaji hodari zaidi bila ya kutegemea watu binafsi na zitakuwa na uwezo wa kuendeleza timu za watoto na vijana kwa ajili ya kuibua vipaji na kulifanya taifa kuwa na wachezaji wa kutosha wenye uwezo.

Wachezaji hao pia watazisaidia klabu nyingine kwa kusajiliwa na Yanga na Simba zitavuna fedha kwa kuwauza.

Kwa vile wachezaji hao vijana watakuwa wameandaliwa kisasa na kisayansi itakuwa rahisi kwao pia kupata timu za kucheza soka na kulipwa nje kwa hiyo watakuwa na mishahara mikubwa na kuzitoa familia zao katika umaskini, pia kuwa na uwezo wa kuwekeza nchini na kuwasaidia vijana wengine kupata ajira na kutatua tatizo hilo.

Kwa kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi, vijana hao watapata maarifa makubwa zaidi na kuwa katika hali nzuri na bora ya kuchezea timu ya taifa ya Tanzania na kuibadili timu hiyo kutoka kwenye unyonge wa kufungwa kuwa timu ya ushindani. Pia wataifa mafanikio makubwa na kuondoa unyonge wa miaka nenda rudi.

Licha ya kwamba nimetumia mfano wa klabu za Simba na Yanga lakini utaratibu huu unaweza kutumika na klabu yoyote nchini na kuweza kupata fedha za maendeleo kwa klabu hiyo.

Kinachotakiwa ni uadilifu na uhakika wa fedha hizo kutoliwa na wajanja wa chache na wapenzi nao kuwa na moyo wa kutoa wakielewa kwamba kutoa ni moyo si utajiri.

Masoud Sanani ni mwandishi wa habari mwandamizi. Amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times ( Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe) na Mwananchi. Alikuwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF). Anapatikana email [email protected] simu 0712-020020.