Bonge la kipa hili hapa Yanga, kusimama langoni Septemba 25

YANGA haijamaliza usajili na bilionea wao Ghalib Mohamed ‘GSM’ anapeleka kilio sehemu yoyote akisikia kuna staa anayeifaa timu hiyo na sasa anashusha kipa mmoja hatari.
Yanga wiki hii itamshusha kipa bora wa ligi ya Mali, Diarra Djigui anayekuja kuwa kipa namba moja wa timu hiyo ya Jangwani katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.
Djigui ambaye anatua Yanga akitokea klabu ya Stade Malien ambao ni mabingwa wa Mali, atasaini mkataba wa miaka miwili na Yanga, Mwanaspoti linafahamu.
Kipa huyo, 26, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Mali iliyoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanaocheza kwenye ardhi ya nyumbani (CHAN) 2020, ni chaguo namba moja la kocha wa Yanga, Mtunisia Nesreddine Nabi ambaye amekuwa akitafuta kipa anayemtaka.
GSM wamchomoa SauzI
Shoo nzima ya kuinasa saini Djigui imesimamiwa na bilionea wao Ghalib Mohamed ambaye ilibidi apande dau ili kumbadili mawazo kipa huyo ambaye alikuwa mbioni kutua katika klabu moja ya Afrika Kusini.
Djigui, ambaye alicheza fainali za Kombe la Dunia la Vijana U-20 (2015) na kuiwezesha Mali kumaliza ya tatu nyuma ya Serbia na Brazil, alikuwa mmoja wa makipa watatu bora katika fainali za CHAN 2020 zilizofanyika nchini Cameroon baada ya kuonyesha kiwango kikubwa hasa kuzuia michomo mikali wakifika fainali na kumaliza wa pili nyuma ya Morocco.
Nabi amekuwa katika vita kubwa na mabosi wa Yanga katika hatma ya kipa yupi abaki naye ambapo Mwanaspoti linafahamu mabosi wa Yanga walikuwa wanataka kuendelea na kipa Mkenya Faruk Shikhalo.
Kocha huyo Mtunisia hakubaliani sana na uwezo wa Shikhalo ingawa ndiye kipa aliyewapa Yanga kombe pekee msimu uliokwisha la Mapinduzi kule Zanzibar.
Awali, Nabi alikuwa anataka kipa aliyesimamishwa na kuondolewa na mabosi wa Yanga, Metacha Mnata asamehewe na arudi kazini lakini mabosi wa Yanga waligomea uamuzi huo wakihofia presha ya mashabiki wao.
Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakipeleka presha ya kuzuia Metacha kurejea ndani ya timu hiyo mara baada ya kuwanyooshea kidole cha kati mwishoni mwa msimu uliopita na saa chache baadaye uongozi wa Yanga ulimsimamisha kisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfungia.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kwamba hatua ya Yanga kutaka kumsajili kipa mzawa Erick Johora limeingia ugumu baada ya klabu yake ya Eigle Noir ya Burundi kuweka ngumu kumuachia.
Yanga ambayo leo itashuka uwanjani kucheza mechi yake ya pili ya Kombe la Kagame imemrudisha nchini Shikhalo kimyakimya aje aitumikie Yanga katika mashindano hayo baada ya kubakiwa na kipa mmoja pekee kinda Geoffrey Magaigwa kutokana na Ramadhan Kabwili kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika mchezo wa kwanza.
Shikhalo ambaye anakubalika na mashabiki wa Yanga mkataba wake na Yanga unafikia tamati mwezi Septemba hatua ambayo iliipa Yanga afya ya kumsitishia mapumziko na kurejea nchini na huenda leo akawa golini.
MAKAMBO KAWAJAZA
Yanga jana mchana ilikamilisha usajili wa nyota wao wa zamani, Heritier Makambo aliyesaini mkataba wa miaka miwili na haraka akaanza kuwajaza kwa kusema furaha itarejea kwa mashabiki wa timu hiyo kuanzia msimu ujao.
Yanga msimu uliopita walikuwa wanapitia wakati mgumu baada ya kutokuwa na mshambuliaji mahiri wa kutupia mabao huku kinara wao wa kufunga akiwa Yacouba Sogne aliyemaliza ligi akiwa na mabao nane tu.
Akizungumza na Azam Tv baada ya kusaini mkataba huo mbele ya Katibu Muu wa Yanga, CPA Haji Mfikirwa, Makambo alisema anajua kabisa timu hiyo inahitaji makombe na amekuja kufanikisha hilo.
“Najua tumeyasubiri mafanikio kwa muda mrefu, ni muda wa kupata makombe na ndio maana nimerudi kuja kuhakikisha tunayapata.” alisema akiongeza: “Nitaendelea na staili yangu ya ushangiliaji kama kawaida ya kuwajaza kama zamani.”
Naye Katibu Mkuu wa Yanga, CPA Haji Mfikirwa alisema usajili wa Makambo sio wa mwisho bali wataendelea kwa kufuata matakwa ya mwalimu wao mkuu, Nabi.
“Nawaomba wana Yanga watulie maana mambo mazuri yanazidi kuja, tunaendelea na usajili tena kwa kasi kubwa vyote ambavyo tunafanya vipo kwenye mipango yetu.
“Haya ni kama matofali ambayo tunayatengeneza kwasasa kuhakikisha tunajenga nyumba kwani hata Roma haikujengwa kwa siku moja na sisi ndio tunaendelea kuijenga Yanga yetu,” alisema Mfikirwa.
Akizungumzia tetesi za kusajiliwa kwa Peter Banda katika klabu yao huku watani zao wa jadi Simba nao wakihusishwa naye, Mfikirwa alisema mchezaji huyo hayupo kwenye mipango yao ya usajili.
“Narudia tena sisi tunasajili kulingana na mahitaji ya mwalimu, inawezekana akawa mchezaji mzuri lakini sisi kwetu hayupo kwenye mapendekezo na hatufanyi vitu kwa hisia, tunaona tu kwenye mitandao,” alisema Mfikirwa.
Makambo mwenye miaka 27 aliifungia Yanga mabao 17 msimu wa 2017-18 na baadaye alitimkia zake Horoya Guinea ambapo hakuwa na wakati mzuri.