Black Sailors yazipigia hesabu nne za kwanza
Muktasari:
- Tedy amesema hadi kufikia sasa, kikosi chake kinatia matumaini, kutokana na maendeleo yanayoonekana mazoezini kwa wachezaji kuwa na utayari kuendelea kufanyia kazi maeneo ya kiufundi na kiushindani kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
ZANZIBAR; KOCHA wa Black Sailors, Mohammed Ali Hilal ‘Tedy’ amesema kikosi hicho kimejikita zaidi kujiandaa kwa ajili ya kuanza vyema msimu wa Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027 kwa kupata matokeo mazuri michezo minne ya kwanza.
Tedy amesema hadi kufikia sasa, kikosi chake kinatia matumaini, kutokana na maendeleo yanayoonekana mazoezini kwa wachezaji kuwa na utayari kuendelea kufanyia kazi maeneo ya kiufundi na kiushindani kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo amesema benchi la ufundi linaendelea kufanyakazi kuhakikisha timu inakuwa tayari kukabiliana na changamoto za ligi.
“Mechi nne za mwanzo ni muhimu kwa timu kupata mwelekeo mzuri wa msimu, hivyo tunahitaji kuwa makini kutumia vyema nafasi tutakazozipata katika kila mchezo,” amesema.
Kocha huyo amesema kikosi chake kinaendelea kujenga hali ya kujiamini na mshikamano na kuwataka wachezaji kuelewa majukumu yao ndani ya mfumo wa timu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, Agosti 31, 2026 Black Sailors itaikaribisha Chipukizi United, mchezo ambao utakuwa kipimo cha kwanza kwa kikosi hicho katika safari ya msimu wa 2026-2027 baada ya kupanda daraja.
Katika mtiririko wa mechi hizo nne pia itacheza dhidi ya Wembe (Septemba 3, 2026), FSC (Septemba 12, 2026) na Mwenge (Septemba 16, 2026).