Bilioni 2.2 kuibadilisha Pugu AFCON 2027
Muktasari:
- Kuhusu changamoto ya barabara za kuingia hifadhini, Kiboko amesema maboresho ya awali yamefanyika, huku fedha zilizotolewa zikitarajiwa kusaidia kuimarisha njia hizo ili ziweze kupitika kwa urahisi, hususan wakati wa mvua na kurahisisha usafiri wa watalii wanaoingia na kutoka katika eneo hilo.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, ameipa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) hadi Aprili 15, 2027, kukamilisha miradi yote ya kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Pugu Kazi Mzumbwi, wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, ikiwa ni maandalizi ya kupokea wageni watakaokuja nchini kushuhudia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Dk Kijaji ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 20, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika hifadhi hiyo, akisema fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zinapaswa kutumika kwa wakati na miradi ikamilike kulingana na ratiba iliyowekwa.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii iliwasilisha maombi ya fedha kwa Rais Samia kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika hifadhi hiyo ili kuitumia kama sehemu ya vivutio vya utalii na burudani kwa wageni watakaotembelea Tanzania wakati wa mashindano hayo ya soka barani Afrika.
“Tunamshukuru sana Dk Samia Suluhu Hassan. Fedha hizo ametupatia zote na tumeshazipeleka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ili aweze kusimamia ujenzi wa miundombinu tuliyoibainisha mapema, ili tuweze kuwapokea wageni wetu na kufurahia mandhari nzuri ya hifadhi hii,” amesema Dk Kijaji.
Alieleza kuwa jumla ya Sh bilioni 2.2 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa kiasi hicho kinapaswa kwenda sambamba na kasi ya utekelezaji ili hifadhi iwe tayari kabla ya kuanza kwa mashindano hayo mwaka 2027.
Waziri huyo amesema amekagua kazi zinazoendelea na kuridhishwa na hatua za awali zilizofikiwa huku akitoa maelekezo zaidi kwa TFS kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi na miundombinu yote inakamilika ndani ya muda uliopangwa.
“Baada ya kuwa tumepewa fedha kiasi cha Sh bilioni 2.2, ni wajibu wetu kuhakikisha miradi yote hiyo inakamilika ndani ya wakati. Nimewaachia maelekezo kwamba ifikapo Aprili 15, 2027, miradi yote iliyopokea fedha iwe imekamilika na tayari kwa mapokezi ya wageni wetu,” amesema.
Ameongeza kuwa maandalizi hayo si kwa ajili ya AFCON pekee, bali pia ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kuongeza idadi ya watalii, kupanua wigo wa vivutio vinavyopatikana nchini na kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Kwa mujibu wa Dk Kijaji, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuibua na kutangaza vivutio vipya vya utalii ili kufikia lengo la kupokea watalii milioni nane kwa mwaka ifikapo 2030.
Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na Naibu Kamishna wa TFS, Emmanuel Kiboko, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma wa wakala huo, akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti Itozya.
Kiboko amesema Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazi Mzumbwi ina ukubwa wa takribani hekta 7,927 na imekuwa ikitumika kwa shughuli mbalimbali za utalii, ikiwemo malazi, mapumziko na burudani kwa wageni kutoka maeneo tofauti ya Tanzania na nje ya nchi.
Amesema TFS imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za hifadhi hiyo, ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni na maeneo ya mapumziko, huku maandalizi ya AFCON yakifungua fursa mpya za kuitangaza hifadhi hiyo kama sehemu ya kutembelea wakati wa mashindano.
“Kwa sasa tumefanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Tutakuwa na sehemu za kuangalia mechi mbalimbali zitakazokuwa zikichezwa nje ya Dar es Salaam. Wale watakaohitaji kuja hapa kuangalia mashindano hayo katika mandhari ya msituni wataweza kufanya hivyo,” amesema Kiboko.
Ameongeza kuwa hifadhi hiyo pia inaendelea kuandaliwa kwa ajili ya kuwahudumia wageni watakaohitaji kupata malazi, akieleza kuwa lengo ni kutumia fursa ya AFCON kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na TFS.
Kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Kiboko amesema baadhi ya kazi zimefikia hatua nzuri, huku baadhi ya nyumba za kulala wageni zikiwa zimekamilika kwa asilimia 100 na nyingine zikiwa katika hatua ya takribani asilimia 70.
Amesema kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wakati wa ziara hiyo, TFS imeanza maandalizi ya kuongeza nyumba nyingine saba za kulala wageni ili kupanua uwezo wa hifadhi hiyo kuwahudumia watalii watakaofika wakati wa AFCON na baada ya mashindano.
Kwa mujibu wa Kiboko, wakala huo unatarajia kukamilisha maandalizi hayo ifikapo Desemba mwaka huu, hatua itakayowezesha kazi zilizobaki kuendelea kwa kasi na kuruhusu ukaguzi mwingine kufanyika kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa na Waziri.
Kuhusu changamoto ya barabara za kuingia hifadhini, Kiboko amesema maboresho ya awali yamefanyika, huku fedha zilizotolewa zikitarajiwa kusaidia kuimarisha njia hizo ili ziweze kupitika kwa urahisi, hususan wakati wa mvua na kurahisisha usafiri wa watalii wanaoingia na kutoka katika eneo hilo.