AFCON 2027; Tanzania yaongeza kasi ya maandalizi
Muktasari:
- Fainali hizo zitakazofanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027, zitaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda kutokana na zabuni ya pamoja iliyofahamika kama Pamoja Bid, hatua itakayorejesha mashindano hayo Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza.
TANZANIA imeongeza kasi ya maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikielekeza nguvu katika ujenzi na ukarabati wa viwanja, kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama na kukijenga upya kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Fainali hizo zitakazofanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027, zitaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda kutokana na zabuni ya pamoja iliyofahamika kama Pamoja Bid, hatua itakayorejesha mashindano hayo Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyotolewa Julai 30, 2026, maandalizi yanaendelea katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha nchi inatimiza masharti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), yakiwemo miundombinu ya michezo, usafiri, usalama na huduma kwa wageni.
VITUO VITATU
Tanzania itakuwa na vituo vitatu vya mashindano, ambavyo ni Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar. Kila kituo kinapaswa kuwa na viwanja vitano vya mazoezi vinavyokidhi viwango vya CAF kwa ajili ya timu zitakazoshiriki fainali hizo.
Dar es Salaam itakuwa kitovu kikuu cha mashindano nchini, huku ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiendelea kwa gharama ya Sh41.7 bilioni.
Kazi hizo zinahusisha kuboresha eneo la kuchezea, sehemu za wageni maalumu (VVIP) na kuweka mifumo ya kisasa ya usalama inayokidhi viwango vya kimataifa.
Serikali pia inaendelea kujenga na kuboresha viwanja vya mazoezi vya Leaders Club, Farasi Arena na Gymkhana 2. Wakati huohuo, viwanja vya Meja Jenerali Isamuhyo, Gymkhana na Shule ya Sheria vimekamilika na kuwa tayari kutumika.
Mkoani Arusha, ujenzi wa uwanja mpya wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 32,000 umefikia asilimia 88. Sambamba na hilo, ujenzi wa viwanja vitano vya mazoezi unaendelea ili kukidhi mahitaji ya CAF.
Serikali pia inaboresha barabara zitakazounganisha uwanja huo na mtandao mkuu wa barabara, hatua inayolenga kurahisisha usafiri wa timu, waamuzi, viongozi wa CAF na mashabiki wakati wa mashindano.
Zanzibar nayo inaendelea na maandalizi yake kwa ujenzi wa Uwanja wa Fumba, wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 36,500, ambao umefikia asilimia 73 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026.
Katika eneo la viwanja vya mazoezi, vitatu vimekamilika huku vingine viwili vikiendelea kujengwa ili kukamilisha mahitaji ya CAF.
Aidha, ujenzi wa Uwanja wa Suluhu Academy wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,470 umefikia asilimia 63, huku ukitarajiwa kukamilika Desemba 2026.
MASHARTI YA CAF
Mbali na ujenzi na ukarabati wa viwanja, Serikali inaendelea kutekeleza masharti ya CAF yanayohusu maandalizi ya mashindano hayo.
Taarifa ya wizara inaeleza Tanzania tayari imelipa ada ya uenyeji ya Dola 30 milioni na imetoa misamaha ya kodi kwa huduma zinazohitajika wakati wa maandalizi na ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa visa ya pamoja kati ya nchi tatu waandaaji.
Mfumo huo unalenga kurahisisha usafiri wa wageni na washiriki kati ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama, kuandaa makao makuu ya Sekretarieti ya CAF katika jengo la JNIC na kuunda kamati za maandalizi kwa kuzingatia miongozo ya shirikisho hilo.
Wakati huohuo, mpango mkakati wa maandalizi ya AFCON 2027 umekamilika kwa kiasi kikubwa, huku kampeni ya kimataifa ya kuitangaza michuano hiyo ikiwa katika hatua za mwisho.
TAIFA STARS YAPEWA KIPAUMBELE
Katika upande wa maandalizi ya timu ya taifa, Serikali na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeendelea kuweka mikakati ya kukiimarisha kikosi cha Taifa Stars.
Mkakati huo unahusisha kutambua na kukuza vipaji vya vijana, kuwatafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje ya nchi na kuwaingiza katika mfumo wa timu ya taifa, pamoja na kuboresha benchi la ufundi chini ya Kocha mkuu Miguel Gamondi.
Lengo ni kuhakikisha Taifa Stars inakuwa na kikosi chenye ushindani wa kutosha kukabiliana na timu bora za Afrika katika fainali zitakazofanyika mbele ya mashabiki wa nyumbani.
KUITANGAZA TANZANIA
Sambamba na maandalizi ya michezo, Serikali imezindua kampeni maalumu ya kuitangaza Tanzania kuelekea AFCON 2027 kupitia kaulimbiu za “Twenzetu Tanzania – Where Africa Belongs” na “Karibu Tanzania – Where Africa Belongs.”
Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi, kutangaza vivutio vya utalii, kuonyesha fursa za uwekezaji na kushirikisha vyombo vya habari pamoja na majukwaa ya kidijitali katika kuitangaza Tanzania na mashindano hayo kimataifa.
Kwa kuunganisha maandalizi ya viwanja, miundombinu, usalama, utalii na timu ya taifa, Tanzania inalenga kuhakikisha inakuwa mwenyeji bora wa AFCON 2027.
Mafanikio ya maandalizi hayo hayatapimwa kwa kukamilika kwa mashindano pekee, bali pia kwa uwezo wa miradi hiyo kuleta manufaa ya muda mrefu kwa michezo, utalii na uchumi wa nchi hata baada ya fainali hizo kumalizika.