Bigman: Kocha kaondoka? Haina noma
Muktasari:
- Nurdin alitangazwa kushika nafasi hiyo akitokea timu ya vijana (U20) akionesha kiwango bora, lakini hajaweza kudumu, huku ikitajwa misimamo yake kuwa sababu kubwa kutimka kikosini.
WAKATI aliyekuwa Kocha Mkuu wa Bigman, Amanzi Nurdin akitangaza kutimka kikosini, uongozi umesema timu hiyo haushtushwi na uamuzi huo kwani imekuwa daraja kwa makocha wengi kuwafungulia milango.
Nurdin alitangazwa kushika nafasi hiyo akitokea timu ya vijana (U20) akionesha kiwango bora, lakini hajaweza kudumu, huku ikitajwa misimamo yake kuwa sababu kubwa kutimka kikosini.
Bigman inashiriki Ligi ya Championship na mechi ya kwanza ilipoteza ugenini mabao 2-1 dhidi ya IAA ya jijini Arusha, huku kesho Jumapili ikiwa kibaruani tena dhidi ya KMC.
Nurdin aliliambia Mwanaspoti baada ya kuona alichotarajia kwenda tofauti, ameamua kutimka na atabaki kama mdau wa timu hiyo kwakuwa hajaondoka kwa shari.
“Kuna mapendekezo niliweka lakini hayakutimizwa hivyo ili kutokuwa sababu yoyote nimeamua kujitoa ili wengine waweze kuendelea, sijaondoka kwa shari na nitakuwa mdau wa timu pale wakihitaji ushauri nitatoa,” amesema kocha huyo.
Mkurugenzi wa timu hiyo, Ahmad Waziri Gao, amesema kuondoka kwa kocha huyo ni mwendelezo na historia ya Bigman kuendelea kuwafungulia milango makocha kwakuwa wengi wamepita na wanaendelea na kazi kwingine.
Amesema kwa sasa timu hiyo itakuwa chini ya nyota wa zamani wa Yanga aliyewahi kuionoa Ken Gold ikiwa Ligi Kuu, Omary Kapilima na matarajio yao uongozi ni kuona Bigman ikipanda daraja.
“Walishapita wengi na wanafanya kazi kwingine kama Zuberi Katwila (Geita Gold), Fred Felix ‘Minziro’ (Fountain Gate), Yusuph Chipo na sasa yeye (Nurdin) ameondoka, hatushtuki, kwa sasa timu iko chini ya Kapilima.
“Siwezi kuongea mengi lakini uongozi una matarajio makubwa kwakuwa Bigman imechoka Championship hivyo tunachotaka ni kuona tunacheza Ligi Kuu na hili linawezekana,” alitamba kigogo huyo.