Safari ya kupanda Ligi Kuu inaanza leo
Muktasari:
- Ligi ya Championship inaanza ikizikutanisha timu zenye historia tofauti kwenye soka hapa nchini, ambapo mwisho wa ligi hiyo, timu mbili za juu zitapanda daraja moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Bara 2027-2028.
HESABU za kupanda Ligi Kuu Bara au kubaki Ligi ya Championship na presha ya kushuka daraja kwenda First League, zinatarajia kuanza leo Ijumaa Septemba 12, 2026 kwa timu nne kushuka uwanjani.
Ligi ya Championship inaanza ikizikutanisha timu zenye historia tofauti kwenye soka hapa nchini, ambapo mwisho wa ligi hiyo, timu mbili za juu zitapanda daraja moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Bara 2027-2028.
Hata hivyo, timu za nafasi ya tatu na nne zitakuchuana kwenye mchujo mkondo wa kwanza ‘play off’ kusaka nafasi ya kupanda, ilhali nafasi ya 15 na 16 zikishuka daraja, huku zile za nafasi ya 13 na 14 zikijitetea kubaki kwenye ligi kupitia mchujo.
Rhino Rangers iliyowahi kushiriki Ligi Kuu Bara, imerejea Championship, ambapo itaanzia nyumbani kuikaribisha Tanzania Prisons iliyoshuka daraja msimu uliopita, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
KMC iliyoshuka daraja msimu uliopita, inaanza kampeni yake kuisaka tena Ligi Kuu itakapokuwa nyumbani dhidi ya Mbuni inayoshiriki Championship kwa msimu wa tano sasa ikisaka ndoto mpya ya Ligi Kuu.
Ligi hiyo inatarajia kuendelea kesho Jumamosi, KenaGold itawakaribisha wageni wa Championship, Bandari Tanzania, huku Kigamboni United ikiwa mwenyeji wa TMA, wakati Stand United ikiipokea Tabora United ambayo awali ilitambulika kwa jina la Mbeya Kwanza.
Jumapili itashuhudiwa IAA iliyotinga Championship ikiumana na Bigman, Transit Camp ikichuana na Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, huku Songea United ikiialika Gunners katika mwanzo mpya.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa, amesema wanafahamu ugumu na ushindani wa ligi hiyo na wanaenda kwa tahadhari dhidi ya wapinzani wao, Rhino Rangers.
“Tunajua wapinzani si wageni kwenye ligi kama ilivyo kwetu, wamejipanga kama tulivyojiandaa, kimsingi ni kuwaheshimu na kuweka nidhamu ya mpira tukiwa na hesabu za kushinda mechi hiyo,” amesema Nsajigwa.
Kocha Mkuu wa Bandari Tanzania, Habibu Kondo, amesema uwezo na uzoefu alionao kwenye soka nchini pamoja na ubora wa nyota wake, anaamini watafanya vizuri kuanzia mchezo huo na kufikia malengo.
Katibu wa Stand United, Fred Masai, amesema mipango iliyowekwa na uongozi msimu huu, hawaoni kukwama kurejea tena Ligi Kuu baada ya kukosa uhondo huo kwa muda mrefu, hivyo azma yao ni kukata kiu ya mashabiki.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa (IRFA), Cyprian Kuyava, amesema baada ya kuinasa TMA, kwa sasa mkakati wao wakishirikiana na wadau wa soka mkoani humo ni kuona wanapata timu ya Ligi Kuu.