Prime
Barker hatanii, kufichua mtego Zanzibar
SIMBA ndio kama ulivyosikia, imeshatinga nusu fainali ya Kombe la Muungano ikitumia kikosi cha wachezaji wengi ambao hawakuwa wanapata nafasi ikishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Mafunzo juzi, lakini kocha wa wekundu hao ametamka kwamba anarudisha jeshi kamili.
Kocha Steve Barker ameliambia Mwanaspoti mchezo uliopita dhidi ya mafunzo alitaka kuwapumzisha wachezaji wake ambao walikuwa wakicheza sana mechi za ligi kutokana na uchovu wa safari ndefu za mechi tofauti.
Barker alisema hata hivyo amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyocheza mechi hiyo na kushinda akisema imelinda malengo yao ya kutaka kushinda kwanza kabla ya kuangalia mengine.
Juzi, Simba iliing’oa Mafunzo kwa bao 1-0 kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Muungano ikitinga hatua ya Nusu Fainali ikienda kukutana na Mlandege ya Zanzibar
“Kitu muhimu tumeshinda hayo ndio yalikuwa malengo ya kwanza, siku zote Simba ikiwa uwanjani matokeo ya ushindi ndio yanahitajika na sio kingine, nawapongeza sana wachezaji wangu kwa hili ingawa hatukutengeneza nafasi nyingi sana,”alisema Barker.
“Tulitumia wachezaji wengi ambao walikuwa hawapati nafasi ya kucheza kwenye ligi, kuna kundi lingine limekuwa likitumika sana kwenye ligi na tukisafiri umbali mrefu, tumewapumzisha ili warudishe utulivu wa mwili.
Barker alisema kuanzia hatua ya nusu fainali timu yake kuna uwezekano mkubwa itashusha mziki kamili kuhakikisha wanakwenda fainali na kuchukua ubingwa wa kombe hilo.
“Nafikiri hatua inayofuata tutakuwa na kikosi tofauti, tutakuwa na timu inayotaka kwenda fainali tunataka kushinda hayo ndio malengo yetu ya kwanza na kuchukua ubingwa huu.
“Tunapokwenda kushiriki mashindano yoyote kama Simba hakuna timu ambayo tutahofia kukutana nayo, tupo sawa kupigania malengo yetu, huwezi kuapata mafanikio kwa kuhofia kupambana na wale walio vizuri.”