Bao la JKT lamshtua kocha Mashujaa Queens
Muktasari:
- Mashujaa Queens imepoteza kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Wanawake uliochezwa leo Septemba 30, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, huku bao hilo la Fatuma Muhubu dakika ya 48 likifungwa baada ya JKT Queens kufanya shambulizi la kushtukiza wakati wapinzani wao wakiwa wamepeleka nguvu nyingi mbele.
KOCHA Mkuu wa Mashujaa Queens, Rajab Ally, amesema bao walilofungwa na JKT Queens limewapa funzo na kubaini maeneo wanayopaswa kuyafanyia kazi, hasa namna ya kudhibiti mabadiliko ya mchezo wakati wa kushambulia.
Mashujaa Queens imepoteza kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Wanawake uliochezwa leo Septemba 30, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, huku bao hilo la Fatuma Muhubu dakika ya 48 likifungwa baada ya JKT Queens kufanya shambulizi la kushtukiza wakati wapinzani wao wakiwa wamepeleka nguvu nyingi mbele.
Rajab amesema tukio hilo limewafundisha umuhimu wa kuwa makini wakati wote wa mchezo, akisisitiza watafanyia kazi makosa hayo kabla ya mchezo wao unaofuata.
“Wakati tunashambulia, tumepigwa shambulizi la kushtukiza na tukaruhusu bao. Hilo ni moja ya jambo ambalo tunapaswa kulifanyia kazi,” amesema.
Amesema licha ya kupoteza, Mashujaa Queens ilicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ndani ya dakika 90, lakini tatizo lilikuwa kushindwa kuzitumia ipasavyo.
“Kwa dakika 90 zote, Mashujaa Queens ilitawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi, lakini tukashindwa kuzitumia kuwa mabao. Kwa upande wangu, tulistahili kushinda mchezo wa leo,” amesema.
Rajab amesema katika kipindi cha pili waliongeza mashambulizi baada ya kuona hakuna sababu ya kuendelea kucheza kwa kujilinda, lakini walishindwa kupata bao kutokana na kutokuwa makini katika hatua ya mwisho ya mashambulizi.
Hata hivyo, amesema hawajakata tamaa kwa kuwa bado wana nafasi ya kuwania nafasi ya tatu, huku akiahidi kutumia mchezo huo kama somo la kurekebisha upungufu uliojitokeza.
Amesema maeneo makuu watakayoyafanyia kazi ni umaliziaji wa nafasi wanazotengeneza pamoja na udhibiti wa mabadiliko ya mchezo, ili kuepuka kuruhusu mabao katika mazingira kama waliyokutana nayo dhidi ya JKT Queens.
Kwa kupoteza mchezo huo, Mashujaa Queens sasa inakwenda kucheza mechi ya kusaka nafasi ya tatu dhidi ya Yanga Princess ambayo nayo imefungwa na Simba mabao 3-0 katika nusu fainali ya pili. Mechi itachezwa Oktoba 3, 2026.