Prime
Aziz KI aja na jipya Yanga
KAMA kuna jambo lililomfurahisha kiungo Stephane Aziz KI katika mechi ya kwanza baada ya kuanza kupewa nafasi, ni kumwona mshambuliaji mpya Peter Shalulile akianza kuzoea mfumo wa timu, huku yeye akianza kutekeleza kile anachokiamini zaidi kutengeneza nafasi za mabao badala ya kufunga.
Aziz KI alikuwa mchezaji wa mwisho kabisa kujiunga na Yanga katika usajili uliopita. Hii ni mara ya pili kurejea katika klabu hiyo baada ya awali kuitumikia na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2023/24 akiwa na mabao 21. Hata hivyo, sasa anasema amerudi akiwa na kazi tofauti na ile aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo, ambaye juzi alicheza mechi yake ya kwanza wakati Yanga ilipopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, amesema kwa sasa kazi yake ni kutengeneza mabao kwa wenzake na tayari ameanza kuonyesha makali yake baada ya kumpa pasi ya bao Shalulile katika mechi hiyo.
“Nilimwambia Shalulile kabla ya mechi ajiandae, kwa sababu sasa muda wake wa kupokea pasi za mabao umefika. Hivyo, washambuliaji watafunga sana mabao msimu huu. Hii ndiyo kazi ambayo nimeichagua na kocha anafurahishwa nayo,” amesema Aziz KI.
Kiungo huyo aliyewahi kuichezea Wydad kabla ya kujiunga na Ittihad ya Libya amesema kila mechi atakayopata nafasi, lengo lake la kwanza litakuwa kuwasaidia washambuliaji wa timu hiyo kupata nafasi za kufunga kwa kuwatengenezea pasi za mabao, kwa kuwa ni jukumu ambalo anaamini anaweza kulitekeleza vizuri.
Anaamini eneo hilo linaweza kumsaidia kuongeza thamani yake ndani ya kikosi, hasa kwa kuwa timu hiyo ina washambuliaji wenye uwezo wa kutumia nafasi wanazotengenezewa.
Burkina Faso international attacking midfielder Stephane Aziz Ki
“Bado sijawa fiti kwa kiwango kinachohitajika, lakini nimefurahi kuanza kupata nafasi ya kucheza mchezo wangu wa kwanza. Ninachotaka ni kuendelea kupata dakika na kurudi kwenye kiwango changu,” amesema.
Kauli hiyo inaweza kuwa habari njema kwa Shalulile, mwenye mabao matatu kwenye ligi, pamoja na Cheikh Toure, mwenye bao moja, ambao wanatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo msimu huu, kwenye ligi na michuano ya kimataifa.
Ikiwa Aziz KI ambaye ni mume halali wa Mwanamitindo Hamisa Mobetto atarejea kwenye kiwango chake kamili cha utimamu wa mwili, kasi yake ya kufungua nafasi na uwezo wa kupiga pasi za mwisho vinaweza kuwa silaha muhimu kwa washambuliaji hao.