Azam FC yatua Misri ikijiandaa kuikabili ZED FC
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Azam FC wakiwasiri jijini Cairo, Misri kujiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Zed itakayopigwa Ijumaa, Oktoba 16, 2026.
Muktasari:
- Kikosi cha timu ya Azam FC kimewasili salama nchini Misri tayari kwa mchezo wake wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ZED FC, utakaopigwa Ijumaa, Oktoba 16, 2026.
Kikosi cha timu ya Azam kimewasili salama nchini Misri tayari kwa mchezo wake wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ZED FC, utakaopigwa Ijumaa, Oktoba 16, 2026.
Azam FC ‘Wanalambalamba’ wamewasili Misri wakiwa na dhamira ya kuanza vizuri kampeni yao ya mashindano ya kimataifa, wakilenga kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza kabla ya kurejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Azam haikushiriki raundi ya awali ya mashindano hayo, kutokana na nafasi yake katika mfumo wa viwango vya klabu za Afrika unaotumiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Azam FC imekusanya pointi tano, ambazo zimeiwezesha kushika nafasi ya 39 Afrika na kupata faida ya kuanzia raundi ya pili ya awali.
Kibarua rasmi kwa timu hiyo kinaanza sasa, ambapo inapaswa kufanya vizuri dhidi ya ZED FC, katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini ili kupata tiketi ya kutinga hatua ya makundi.
Upande wa ZED FC, inaingia katika mchezo huo ikiwa imetoka kushiriki raundi ya kwanza ya awali, ambayo ilifanikiwa kuiondoa ASAS Djibouti Télécom kwa jumla ya mabao 5-1.
Hali hiyo inaifanya mechi ya Ijumaa kuwa mtihani mgumu kwa Azam FC, ambayo italazimika kuonyesha nidhamu ya kiufundi, uimara wa safu ya ulinzi na umakini katika kutumia nafasi za kufunga ili kupata matokeo yatakayoipa faida kuelekea mchezo wa marudiano.
Kwa upande mwingine, ZED FC itakuwa na dhamira ya kutumia faida ya kucheza nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya kwenda kwenye mchezo wa pili.