Aussems: Morrison Yanga atacheza

MAKOCHA wa zamani wa kigeni wa Simba na Yanga wamesema kwamba Bernard Morrison aliyepumzishwa na Simba mpaka mwisho wa msimu ana nafasi kwenye kikosi cha Jangwani kama akitulia.

Patrick Aussems ‘Uchebe’ ambaye aliinoa Simba kwa mafanikio na sasa yupo AFC Leopards ya Kenya, alisema Morrison ni mchezaji mzuri na mzoefu na mashindano ya kimataifa akituliza kichwa ana nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza cha Yanga.

“Mpira unachezwa uwanjani mchezo anaweza kuwa na nidhamu mbovu lakini akiwa uwanjani anafanya kazi nzuri kama wana uhaba wa mchezaji wa nafasi hiyo na kocha kapendekeza kusajiliwa winga anaweza akawasaidia japo wana machaguo mengi wanaweza kutoka na kwenda kusaka nje ya ligi wanayoshiriki,” alisema na kuongeza;

“Kwa kumfuatilia kiwanjani naiona nafasi yake ndani ya kikosi cha Yanga, ni winga mzuri anaweza kukaa na mpira mguuni ana kasi anamlazimisha mpinzani kumfuata alipo kwa kujiamini, ni mchezaji bora akipata kocha ambaye ataweza kumtumia vizuri,” alisema.

Luc Eymael ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga aliyemleta staa huyo nchini alisema inahitaji akili ya ziada kummudu Morrison licha ya kuwa na kipaji kikubwa ambacho kinaweza kumpa namba kwenye klabu yoyote Afrika.

“Nilifanya naye kazi vizuri pamoja na kwamba kuna muda nilikuwa nikikwaruzana naye, lakini alikuwa mchezaji mzuri, hakuna kocha ambaye anaweza kumweka benchi Morrisson akiwa kwenye ubora wake, ni mwepesi wa kunusa na kuleta madhara, kinachomwaribia ni matukio yake mengine nje ya uwanja,” alisema kocha huyo ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwao Ubelgiji.

Eymael amezisikia taarifa za winga huyo kuwekwa kando wa waajiri wake huku kukiwa na uvumi kuwa huenda akarejea Jangwani, “Lolote hutokea kwenye maisha ya mpira.”

Mchambuzi wa soka George Ambangile alisema hawezi kushangaa kumuona Morrison akirudi tena Yanga kwasababu ndio levo za timu za Tanzania kufanya usajili wa aina hiyo hawawezi kushindana na timu kubwa za Afrika.

“Al Ahly, Mazembe na klabu nyingine kubwa ambazo zimewahi kutwaa mataji Afrika wana bajeti kubwa wanaweza kumsainisha mchezaji kwa gharama kubwa lakini timu zetu Simba na Yanga bajeti zao ndogo hivyo kusajili mchezaji kama Morrison ni kawaida,” alisema.

Morrison alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu uliopita, baada ya kumaliza mkataba wake na Young Africans licha ya kuibuka kwa sintofahamu kati yake na viongozi wa klabu hiyo ambayo ilimleta nchini wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu wa 2019/2020