Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afichua siri ya ushirikina kwenye masumbwi, yeye ni muumini wa hili

JANA Jumamosi katika mfululizo wa makala haya ya bondia wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka alieleza kwa undani jinsi biashara ya kuuza chupa ilivyomwezesha kupiga mijengo miwili ya maana tu. Pia, alieleza michezo michafu ya kuuza mapambano inavyofanyika na kisa cha kutapeliwa mkwanja wake Euro 6000 (zaidi ya Sh 15 milioni) kule Ujerumani.

Pamoja na hivi karibuni, Francis Cheka kupigwa na Abdallah Pazi (Dullah Mbabe), lakini enzi zake Cheka alikuwa kiboko ulingoni, hakuna bondia wa Bongo aliyejipendekeza na kutoka salama ulingoni. Leo Cheka atafunguka siri zote ikiwa ni pamoja na mbinu alizotumia kuwanyamazisha mabondia waliokuwa na umaarufu mkubwa hapa Bongo.

Unajua kwenye masumbwi nako kuna ushirikina tena uliovuka mipaka? Hapa Mwandishi wetu Imani Makongoro aliyemzukia Cheka kule Mtwara na kuzungumza naye:

Si Mada Maugo, Japhet Kasepha, Karama Nyilawila wala Thomas Mashali (marehemu) wote walipigwa tena wengine zaidi ya mara moja, ikafikia mahali mmoja wao akicheza na Cheka wote wanaungana na kuwa kitu kimoja, lakini bado hawakufua dafu kwa bondia huyo bingwa wa zamani wa dunia wa WBF.

“Nakumbuka pambano langu na Kaseba, kama sio vurugu kutokea basi nilikuwa namuua yule. Wakati ule nilikuwa fiti sana, hata Maugo pia, bondia ambaye alinipa upinzani alikuwa Mashali, sababu alikuwa sugu hata umpige ngumi gani, harudi nyuma. “Pambano langu la kwanza kucheza naye, nilimpiga KO sababu pumzi ilikata, hakuwa amezoea kucheza raundi 10, mapambano yake mengi aliishia raundi 10, ndiyo sababu alichoka raundi ya 11, lakini ndiye bondia ambaye ki ukweli alinipa ushindani.

Bondia huyo anasema kilichokuwa kikimbeba kwenye ngumi ni nidhamu ya mchezo, aliheshimu sana mchezo huo na alikuwa akimsikiliza kocha wake Comando kila alichomwelekeza.

“Nilikuwa natoka nyumbani kwangu miezi mitatu kabla ya pambano nakwenda kuishi kwa kocha, au tunapanga chumba na kocha maisha yetu yanakuwa ni mazoezi tu.

“Kocha wangu sio Comando jina, ni Comando kweli, alikuwa akinifundisha ngumi za kuua mtu, nikiwa najiandaa na pambano lazima nijifue kutwa mara tatu.

“Ikiwa siku ya sparing (mazoezi ya ana kwa ana) huwa naomba kupigana na mabondia watatu mpaka wanne kwa wakati mmoja, nilikuwa napigana hadi masparing patner wangu wanaomba po!. “Hivyo ninapokwenda katika pambano, nakuwa kama Chui, nakuwa na uwezo wa ajabu, ndiyo sababu nilikuwa nashinda mapambano mengi.

SIRI YA USHIRIKINA KWENYE NGUMI

Cheka ni miongoni mwa watu wanaoamini uchawi upo, lakini haamini kama unaweza kukusaidia ulingoni kushinda.

“Kwanza ujiandae, hata ukiroga bila mazoezi ni kazi bure, binafsi nilikuwa na kawaida kabla sijapanda ulingoni, lazima nisome dua, japo mimi ni mkristo lakini mke wangu ni muislamu na nilikuwa nikiamini kama ni sehemu ya kumwomba Mwenyezi Mungu anisaidie.

Anasema hakuna bondia, ambaye anaweza kufanikiwa kwa kutegemea kuroga ulingoni ili ashinde, japo hata yeye baadhi ya mabondia aliokuwa akiwapiga waliwahi kudaia anawaroga. “Kama ingekuwa ukiroga unashinda basi tungekuwa hatuna sababu ya kufanya mazoezi, mchawi namba moja ni maandalizi, kipaji na kujituma, hayo mengine mbwembwe tu.

MSOSI WAKE KABLA YA PAMBANO

Kibongo Bongo mabondia wengi hawana utaratibu wa kupangiwa ni chakula gani ale, avae raba za aina gani ulingoni, ataingia vipi, anyoe vipi siku ya pambano au apande ulingoni na swaga gani kama Ulaya.

Hivyo Cheka naye anasema hakuwa na utaratibu huo zaidi ya kujisikia tu kula chakula chochote ambacho atapenda kula siku hiyo, hata ugali na dagaa kama atakuwa amejisikia kula atafanya hivyo.

Ingawa anasema kwenye mavazi na namna ya kuingia ulingoni huwa anajipanga kulingana na pambano, kama ni kubwa ataanzaa raba kali, bukta ya kisasa na hata joho atakaloingilia ulingoni.

Amleta Botha nchini

Pambano la Cheka na Mmarekani, Phil Williams la Agosti, 30 2013 ndilo lilimleta nchini kwa mara ya kwanza bingwa wa dunia wa uzani wa juu, Francis Botha, bondia huyu ‘Heavy weight’ aliambatana na viongozi wa World boxing Federation wakiongozwa na rais wao, Goldberg Haward.

Kwenye Ukumbi wa Diamond Jubillee, Cheka aliwafurahisha Watanzania kwa kumchapa Williams na kutwaa taji hilo la dunia, pambano ambalo lilishuhudiwa na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa kiingilio cha Sh150,000 VIP.

“Lilikuwa pambano lililonipa heshima kubwa kwa viongozi wa serikali, Mtaka (Anthony aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero sasa ni mkuu wa mkoa wa Simiyu) alinipa kiwanja, mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati ule Bendera (Joel sasa ni marehemu) pia alinipa kiwanja.

“Nilipewa mapokezi makubwa na watu wa Morogoro, nilikuwa na ndoto kubwa kwenye ngumi, lakini ghafla ziliyeyuka, tena kinachoniumiza, pesa yangu mwenyewe ndiyo ilisababisha ndoto zangu za ngumi kuyeyuka.

Ilikuwaje hadi pesa zake ambazo amevuna kwa jasho ulingoni ndio zikazima ndoto za maisha yake? Unajua Cheka alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na maisha ya huko yalikuwaje na vipi familia yake huku nje? Fuatilia kesho Jumatatu ufahamu kwa undani zaidi.