Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Straika Muivory aipasua Yanga

KELELE za mashabiki wa soka hasa wale wa upande wa pili, wanaoiponda Yanga kwa kushindwa kupiga dozi ya maana kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara ni kama zimewaamsha mabosi wa klabu hiyo, ambapo kwa sasa akili zao ni kusuka kibabe safu yao ya ushambuliaji.

Katika kuonyesha kuwa mabosi hao wamepania hasa katika kuhakikisha msimu huu wanabeba ndoo waliyoitema misimu mitatu mikononi mwa watani wao, kwa sasa tayari mikononi mwao wana majina matatu ya washambuliaji katika meza yao na wote wakiwa na moto katika kufunga.

Hata hivyo, straika Muaivory Coast anaonekana kuwapasua zaidi kiasi cha mabosi hao kuanza kuchekesha akili kuhakikisha wanambeba kama mipango yao itaenda sawa.

Ripoti ya kocha Cedric Kaze inataka watu wasiozidi wawili katika dirisha hili dogo la usajili lililofunguliwa jana na mabosi wanapambana na mshambuliaji Gbagbo Junior Magbi.

Magbi yupo pale katika kikosi cha Mabingwa wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad Casablanca ya Morocco ambayo sasa ni kama inasuka upya safu yao ya ushambuliaji ikimnasa nyota wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva aliyetokea timu ya Difaa El Jadida.

Maboresho hayo ya kikosi cha Wydad ndio ambayo Yanga inataka kuyatumia kumsomba Magbi ambapo kocha wake mkongwe Faouzi Benzarti anataka kumuachia mshambuliaji huyo baada ya Msuva kutua kikosini hivi karibuni.

Wydad wanataka Magbi atafute timu ya mkopo kutokana na kubakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu katika kikosi hicho, wakati huu wakiangalia maingizo mapya katika timu yao.

Tayari Magbi ameshatakiwa kutafuta timu na haraka jina lake likatua kwa mabosi wa Yanga ambapo baada ya bajeti yake kutua mezani kwa matajiri wa klabu hiyo ya Jangwani wakashika vichwa wakiulizana watapataje huduma yake.

Mwanaspoti linafahamu kwamba mabosi wa GSM chini ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said baada ya kutafuta taarifa za ubora wa Magbi wamekubali kipaji chake katika kufunga lakini pia kasi yake akiwa uwanjani.

Hata hivyo, ugumu wa kumpata Magbi unaonekana katika dau lake ikielezwa akitaka dau kubwa kiasi cha dola 120,000 (Sh 277 milioni) kama ada ya usajili kwa mkataba wa miaka miwili lakini pia mshahara usiopungua Sh 13.8 milioni.

Ugumu mwingine katika dili hilo ni kutokana na meneja wake kutamani kumbakiza mshambuliaji huyo katika ardhi ya Afrika Kaskazini ambako watavuna fedha nyingi ambapo kwa Yanga watamnasa tu endapo watakubali ofa hiyo.

Kama Magbi atanaswa itampa kazi Kocha Kaze kuangalia kati yake na Wakongo wawili akiwamo Dark Kabangu kutoka DC Motema Pembe ambao majina yao tyari yapo mezani kwa mabosi wa Yanga nani aingie kikosini kabla ya dirisha kufungwa Januari 15.

Kwa sasa Yanga imekuwa kwenye wakati mgumu wa kutupia nyavuni kwa kupata ushindi kiduchu, huku mabao mengi yakiwa yamefungwa na wachezaji wa nafasi nyingine wakiwamo mabeki na viungo huku, washambuliaji wake, Michael Sarpong na Yacouba Songne, wakiwa ndio kwanza wanaanza kushika kasi, wakati Ditram Nchimbi na Wazir Junior wakisuasua hata kupata nafasi kikosini.

Simba ndio klabu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi katika ligi mpaka sasa ikiwa imefunga 33 (hii ni kabla ya mechi yao ya usiku wa jana dhidi KMC).