Nabi: Wanapigika kabisa

KIKOSI cha Yanga kinarudi kambini leo haraka tayari kwa maandalizi kuelekea mechi dhidi ya Simba lakini kocha wao Nasreddine Nabi amewaambia wachezaji wake Mnyama anapigika kabisa ila si kwa staili waliyocheza na Namungo juzi.
Amewashushia mkwara mzito wachezaji wake na anataka leo kuwaweka kitimoto wote kila mmoja aelewe kwamba hii mechi haihitaji masihara hata sekunde moja.
Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema amefurahia ushindi ambao Yanga imeupata wakivunja mwiko wa kutowahi kuifunga Namungo lakini kuhusu ubora akaukataa akisema hawakucheza kwa ubora na walitakiwa kushinda nyingi.
Nabi alisema kiwango cha timu yake kimemshtua na kwamba kama wakicheza kwa ubora kama huo katika mchezo dhidi ya Simba Aprili 30 basi wanaweza kupoteza vibaya au kushinda bila mchezo wa kuvutia uliozoweleka na mashabiki.
Kocha huyo alisema mechi dhidi ya Simba ina ujazo mkubwa wa ambapo makosa ya kuwarudisha mchezoni wapinzani sio kitu kinachotakiwa kujirudia wikiendi ijayo huku akiwatoa hofu mashabiki kwamba kila kitu kiko ndani ya muda na anajua nini cha kufanya.
“Tumeshinda sawa nimewapongeza wachezaji na hata wenzangu ambao walikuwa pale kwenye benchi lakini sijafurahia ubora ambao tumeonyesha umenishtua sana hasa wakati huu tunakwenda kukutana na Simba,”alisema Nabi ambaye ana uraia pacha wa Ubelgiji na Tunisia.
“Hatukucheza kwa ubora mkubwa kama Yanga tunavyotaka, tunatoa nafasi ya kumrudisha mpinzani kurudi mchezoni hili ni baya, makosa mengi ambayo tumeyafanya dhidi ya Namungo kama yatajirudia kwenye mechi ijayo tutakimbiana,”alisema Kocha huyo ambaye atakuwa jukwaani kutokana na adhabu lakini amesisitiza mazoezini na kambini ataweka kila kitu sawa kuanzia leo.
Kocha huyo aliongeza kuwa kikosi hicho kinaporudi kambini leo anataka kuzungumza na wachezaji wote kuhakikisha wanarudi katika nidhamu yao kubwa ya kutamani ushindi mkubwa.
Alisema Simba ni timu bora inayotoka kucheza mechi zenye nguvu na kwamba timu yake lazima iwe na ubora mkubwa kupata matokeo ya ushindi ambao ni malengo yao makubwa.
“Tunatakiwa kuifunga Simba hili ni jambo ambalo tulishakubaliana na wachezaji na timu nzima lakini kuna mambo lazima tubadilike, tunakwenda kukutana na timu kubwa yenye wachezaji bora ambao kama ukifanya makosa hawataweza kukuacha salama kirahisi, wana wachezaji walio komaa(Simba),”aliongeza Nabi ambaye amecheka kusikia mtaani wanamuita Profesa.
Aidha Nabi alifurahia kuingia kambini na wachezaji wake wote wakiwa hakuna anayekosa kwa kuwa na kadi wala majeruhi akisema beki Djuma Shaban hana shida ya kukosa mchezo huo.
“Tunaingia katika maandalizi ya mechi hii tukiwa na kundi kamili la wachezaji, tulimpumzisha Job (Dickson) kutokana na alikuwa na kadi mbili za njano kama angepata kadi ingetupa shida, lakini Feisal (Salum) na Aucho (Khalid) nimefurahi jinsi walivyorejea na kucheza kwa utimamu mzuri.
“Mtu aliyebaki ni Saido (Said Ntibazonkiza) ambaye naamini tunapoingia kambini kesho (leo) atakuwa tayari kwa mchezo huo, huyu ni mchezaji mkubwa ambaye ni muhimu kuwa naye katika mechi kubwa kama hii inayokuja,”alisema.
GARI MPYA
Matajiri wa Yanga wamempa nguvu zaidi kuelekea mechi ya Simba wakimpa gari mpya ya kisasa baada ya kujiridhisha kwamba ubingwa uko ndani ya mikono yao.
Nabi juzi alitua Uwanja wa Mkapa akiwa na gari mpya ya kisasa aina ya Toyota Vanguard ambayo amepewa na tajiri wao GSM lakini pia hata wasaidizi wake wawili Helmy Gueldich ambaye ni kocha wa mazoezi ya viungo na daktari wa viungo Youssef Mohamed nao wanachukua yao ndani ya wiki hii.