Mauya: Tulieni mambo bado
KWA jinsi walivyotengenezwa pacha kali, wakicheza kwa mara ya kwanza viungo wa Yanga, Zawadi Mauya na Abubakar Salum ‘Sure’ imekuwa ndio habari ya mjini kwa mashabiki wao.
Mwanaspoti halikuwa nyuma kuwasaka mastaa hao, ili kuzungumzia hilo na namna walivyoona wao wakiwa uwanjani, walikuwa na haya ya kusema.
Sure Boy alisema “Naweza nikacheza na yeyote Yanga, nilivyofurahia kuanza vyema Kombe la Mapinduzi na Mauya ambaye tukajikuta tunaelewana na tunacheza kwa kufurahia, bado ni mapema acha tuone mbele itakuaje,” alisema.
Naye Mauya alimwelezea Sure Boy ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa wa kusoma mchezo na kujua nini kifanyike kwa wakati gani. “Sure Boy alikuwa anarahisisha pasi, tukajikuta tunabondi, lakini bado ni mapema acha tuendelee kupambana tuone kitafanyika nini Mapinduzi na ligi kwa ujumla,” alisema.