Mamia wajitokeza kumuaga mwandishi Joyce Mmasi

Muktasari:

  • Katika shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja ziliambata na salamu kutoka makundi mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali.

 Mamia ya waombowaombolezaji pamoja na waandishi wa michezo wamejitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa Mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, marehemu Joyce Mmasi.

Katika shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja ziliambata na salamu kutoka makundi mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali.

Akiogoza ibada ya kuaga mwili huo Mchungaji wa Kanisa la KKKT Usharika wa Mbezi Luis, Richard Lucas amesema maisha aliyoishi marehemu iwe fundisho kwa waliobaki maana maisha ya mwanadamu ni mafupi.

"Binadamu sisi tunamaisha mafupi ya kuishi duniani na maisha aliyoishi Joyce yalikuwa maisha ambayo aliyakabidhi kwa Yesu hivyo hakuna shaka kuwa marehemu yuko mahali salama," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi, Francis Nanai, Mhariri Mkuu Mtendaji, Bakari Machumu amesema marehemu mbali na kuwa mwandishi lakini pia alikuwa mjasiriamali.

" Hili ni fundisho kwetu kwamba tunahitaji kuishi maisha ya kujiongeza maana Mmasi alikuwa mwanachama mzuri wa Saccos yetu ya Mwananchi na alitoa mawazo ambayo wamesaidia maendeleo ya saccos na kampuni,"amesema.

 

Marehemu amesafirishwa leo Kuelekea kijijini kwao Mbokomu Moshi na anatarajiwa kuzikwa kesho.