Malota : Nilisajiliwa kwa mshahara wa sh200 tu!
Malota
Muktasari:
Pia huwa wanajiangalia jinsi walivyokuwa wakihenyeka wakicheza kwa nguvu zao kiasi cha kutokwa jasho na damu, lakini hawakupewa thamani inayostahili.
WAKATI mwingine nyota wa zamani wa soka hutamani miaka irudi nyuma, ili angalau wanufaike na vipaji vyao. Wanaamini jasho lao lililovuja uwanjani enzi wakicheza halikulingana na kile walichokuwa wakivuna kama shukrani kwa kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya.
Pia huwa wanajiangalia jinsi walivyokuwa wakihenyeka wakicheza kwa nguvu zao kiasi cha kutokwa jasho na damu, lakini hawakupewa thamani inayostahili. Hali ni tofauti na sasa ambapo wachezaji wanaopapatikiwa na kuthaminiwa kupita kiasi, huwa hawana jipya uwanjani, Wanacheza zaidi soka la mdomoni na kwenye magazeti, lakini mwishowe wanavuta mkwanja mnene ambao umewafanya watembee kifua mbele na mabega juu kabla ya kuzimika kimyakimya.
Simba miaka zaidi ya 20 iliyopita iliwahi kuwa na straika matata, aliyekuwa na kipaji cha pekee cha kulichezea gozi la ng’ombe na kuwatungua makipa hodari, kiasi cha mashabiki kumpachika jina la ‘Ball Juggler’. Baadhi nahisi wanatabasamu! Wanamkumbuka sana, mkali huyo aliyefahamika kama Malota Soma.
Katika mahojiano yake maalum na Mwanaspoti, mkongwe huyo ambaye kwa sasa anashughulika na biashara ya kuendesha taksi akimiliki magari yake mwenyewe, anasimulia namna alivyosajiliwa kwa samani za nyumbani (Furnitures) na kulipwa mshahara wa Sh.200. Hujakosea sh.200 tu!
Ilikuwaje?
Nyota huyo wa zamani anasema anakumbuka ilikuwa mwaka 1981, aliposajiliwa Simba akitokea Tumbaku ya Morogoro, mji uliokitambulisha kipaji chake kwa kuzichezea timu mbalimbali zikiwamo Jogoo FC na Reli-Morogoro.
“Nilipewa fenicha kama kitanda, kabati ya vyombo na nguo na meza ya kujipambia (dressing table), ikiwa kama ada ya usajili, sikupewa fedha yoyote, ila niliona ni jambo jema,” anasema.
“Mshahara wangu ulikuwa sh 200, ingawa kwa wakati huo niliweza kujenga nyumba, pia nilisomesha ndugu zangu. Lakini mwaka 1995 nilipokuwa nikimaliza kazi yangu Simba, mshahara ulikuwa ni sh 3,000,” anasema.
Anasema licha ya kwamba kipindi akicheza Tanzania ilikuwa na washambuliaji wakali wakiwamo aliokuwa akicheza nao ndani ya Simba kama akina Edward Chumila, Zamoyoni Mogella, Sunday Juma ‘Pikipiki’, Zubeiry Magoha na wengine, lakini alimudu kwenda nao sambamba kwa vile kipaji chake ni cha kuzaliwa na alikuwa muumini mzuri wa nidhamu na miiko ya wachezaji.
Mechi asiyoisahau
Pengine ungeweza kudhani Malota angetaja mechi za watani, Simba na Yanga kama asizoweza kusahau, lakini yeye anaitaja ile ya mwaka 1985 ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kati ya chama lake la Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Anakumbuka mchezo huo ulipigwa CCM Kirumba, Mwanza ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Malota anaukumbuka mchezo huo mpaka leo kwa sababu, licha ya kutofunga bao lolote siku hiyo, lakini anatamba kuwa yeye ndiye aliyetoa pasi kwa wafungaji wa mchezo huo ambao ni Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ aliyefunga la kwanza na Mtemi Ramadhani aliyemaliza udhia.
Anasema ushindi huo wa Simba uliondoa ile dhana iliyokuwa imejengeka miongoni mwa wadau wa soka nchini kuwa timu za Tanzania haziwezi kuzifunga timu za Misri.
Golden Boy
Malota anasema ni vigumu mno kulinganisha soka la enzi zao na soka la sasa la Simba, kwani mbali na yeye kuonyesha kiwango, wachezaji wengine wa Simba wa enzi hizo walikuwa na kiwango cha hali ya juu.
“Kipindi hicho wakati nacheza soka katikati kulikuwa na washambuliaji wenzangu wawili ambao pia walikuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao kama mimi. Hapa namzungumzia Mogela na Edward Chumila (marehemu).
“Washambuliaji hao walikuwa na uwezo wa kupachika mabao kama ilivyokuwa mimi.”
Anasema mwiba mkali kwa mabeki wa timu pinzani kwa wakati huo alikuwa ni Mogella maarufu kama Golden Boy ambaye anamtaja kama mmoja wa washambuliaji waliokuwa watundu wa kuchezea mpira na asiyetabirika uwanjani katika kufumania nyavu.
“Huyu jamaa alikuwa mtundu na mjuzi haswa, hakupewa jina la Golden Boy kwa bahati mbaya, waliomshuhudia wanatambua umahiri wake, ingekuwa enzi hizi mabeki wengine wangetimuliwa katika klabu zao kwa tuhuma za hujuma kwa namna alivyokuwa wakiwaaibisha mabeki.”
Sasa Zamani
Malota anakiri kuwa soka la zamani na sasa ni kama mbingu na ardhi kutokana na ukweli miaka ya nyuma wachezaji walikuwa wakijituma na kuwa na vipaji halisi na walijua kipi ambacho wanatakiwa kufanya uwanjani, mbali na kile wanacholishwa na makocha wao.
“Zamani wachezaji walijituma kwenye mazoezi na kwenye mechi. Sheria za soka kwa sasa zilikuwa ngumu, waamuzi walikuwa wagumu lakini sasa hivi sheria na kanuni za soka ni tofauti na zinatengenezea wachezaji mazingira mazuri ya kucheza haswa kwa urahisi.
“Pia maisha ya sasa ya wachezaji ni mazuri ukizingatia kuwa timu nyingi zinapata ufadhili na tena makampuni mengi yameingia kwenye soka hivyo wachezaji wote wamekuwa wakinufaika. Zamani kulikuwa na wafadhili, waliokuwa wanachagua nani wa kuwapa pesa kutokana na mapenzi ya wenyewe,” anasema.
Malota anatoa wito kwa wachezaji wa sasa akiwataka wajitume, kwa maelezo kuwa soka la siku hizi linalipa kuliko enzi zao.“Wakati ule ninacheza mpira hakukuwa na fursa kama za siku hizi za kimtandao. Sisi wakati ule tuliwatambua wachezaji wanzetu wa nje kwa kuangalia tu kipande cha gazeti hivyo tuliwajua tu kwa sura na kuwasoma tu na si kuwatazama kwa kutumia luninga kama ilivyo sasa.
Malota Soma alistaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 1999 na klabu ya mwisho kuichezea ilikuwa ni Tanzania Stars. Anasema kuwa aliamua kustaafu kucheza soka ya ushindani ili kuwaachia vijana chipukizi waonyeshe vipaji vyao.
Itaendelea