Klopp kila kitu freshi kwa Werner
LIVERPOOL, ENGLAND. DILI limefika patamu. mwandishi wa habari maarufu, Raphael Honigstein amefichua kila kitu kinachoendelea baina ya kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp na straika wa RB Leipzig, Timo Werner.
Wawili hao wameripotiwa kuwa kwenye mazungumzo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi pamoja huko Anfield wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye Bundesliga msimu huu, Werner amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda Liverpool kwenye dirisha la majira ya kiangazi la baadaye mwaka huu.
Liverpool imeripotiwa kwamba ipo tayari kulipa kiwango cha pesa kinachohitajika kuvunja mkataba wa mshambuliaji huyo na Honigstein amesisitiza kwamba Klopp na Werner wameshafanya mazungumzo juu ya mpango huo.
Honigstein alisema: “Hadi sasa Liverpool wamejisogeza karibu zaidi kwenye mpango wao wa kumsajili Werner na ameshazungumza na Jurgen Klopp wiki chache zilizopita.
“Kitu ambacho kinawazuia hadi sasa hawajatoa pesa ya kuvunja mkataba wake bado hawajapata uhakika mkubwa kwamba tatizo hili la kiuchumi lililosababishwa na corona litamalizika wakati gani, hasa Ligi Kuu England ikitarajia kurejea tena mwezi ujao.
Nadhani wanasubiri tu mambo yawe sawa na dirisha litakapofunguliwa. Lakini, dili kama hizi ni zile ambazo zimekuwa zikitangazwa Aprili au Mei, lakini kutokana na corona itabidi zisubiri Agosti au Septemba. Uhakika ni mkubwa atakwenda Liverpool.”
Werner alifunga hat-trick dhidi ya Mainz 05 juzi Jumapili na hivyo kufikisha mabao 28 kwenye Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.