Huko Yanga kumekucha
HUKO Yanga kumekucha. Kocha wa Yanga, Cedrick Kaze jana amefanya mazoezi kwa siku ya pili na kikosi chake wakirejea kutoka mapumziko huku akisisitiza vijana wake wako vizuri.
Kaze juzi Jumatatu alitumia mazoezi ya jioni kusoma hali ya wachezaji wake, ingawa walikuwa wachache mazoezini kutokana na baadhi kuwa na timu ya Taifa.
Kabla ya kuanza kwa kambi ya juzi, Kaze aliwarudisha nyumbani Carlos Carlihnos, Mukoko Tonombe, Haruna Niyonzima, Farouk Shikalo na wengine baada ya kuchelewa kuripoti kambini mchana kwa dakika kadhaa.
Lakini habari za uhakika Mwanaspoti ilizozipata jana kambini ni wachezaji hao walirejeshwa na kupewa onyo kali na baadae wakaendelea kupiga mzigo. Jana mchana kila mmoja aliwahi kambini haraka.
Kaze akizungumzia kambi alisema wachezaji wamerejea na morali kubwa na ana uhakika ndani ya muda mfupi kulingana na programu atakayowapa watakaa sawa na kabla ya mechi inayofuata watakuwa tayari.
Alisema pia majeruhi Saido Ntibazonkiza na Yacouba Sogne hali zao ziko vizuri na wamerejea mzigoni tayari kwa mapambano.
Kaze alisitiza anatambua mzunguko wa pili utakuwa mgumu na wenye vurugu nyingi za ubingwa ndio maana anakinoa kikosi chake kwa nguvu kubwa ili kiwe tayari kuendeleza rekodi yake.
“Tuna imani mpaka kwenye mechi ijayo wachezaji watakuwa vizuri, tutapata wakati mzuri sana wa kujiandaa na mechi ijayo ya ligi. Yacouba na Saido hii wiki watakuwa kwenye hali nzuri, ukitoa wachezaji walioko kwenye timu za Taifa wachezaji wengine wote wako vizuri kisaikolojia tayari kupambana,” alisema.
Yanga imethibitisha kumwajiri mchezaji wao wa zamani, Nizar Khalfan kuchukua nafasi ya Kocha msaidizi Juma Mwambusi.
Lakini Mwanaspoti linajua kuna wataalamu wengine watatu aliopendekeza Kaze ambao ni kocha wa viungo, mchua misuli na daktari ambao muda wowote watamalizana na Yanga na kujiunga kambini.
FISTON KESHO
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni straika mpya, Fiston Abdul Razak anatua nchini kesho saa 6:30 mchana akitokea kwao Burundi.
Staa huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika inadaiwa amechelewa kufika kutokana na ishu za Corona ambazo zimeathiri miundombinu mingi ya usafiri nchini kwao.
Yanga ilisajili majembe matatu kwenye dirisha dogo ambayo ni Dickson Job ambaye ni beki na mastraika, Saido na Fiston na wachezaji kadhaa wa timu ya vijana wakapandishwa.