Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar ilivyoshindwa kutamba AFCON Kabaddi 2026

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Nafasi ya pili ya mashindano hayo imechukuliwa na Uganda iliyoanza vizuri lakini mwisho ikashindwa kufanya kweli, huku Tanzania Bara ikifanikiwa kuwa ya tatu, wakati Zanzibar iliyokuwa mwenyeji ikiondoka patupu.

ZANZIBAR; MICHUANO ya Afrika ya Kabaddi kwa Wanaume (AFCON Kabaddi 2026), imemalizika kwa timu ya Kenya kuwa bingwa baada ya kuifunga Uganda pointi 35-21.

Nafasi ya pili ya mashindano hayo imechukuliwa na Uganda iliyoanza vizuri lakini mwisho ikashindwa kufanya kweli, huku Tanzania Bara ikifanikiwa kuwa ya tatu, wakati Zanzibar iliyokuwa mwenyeji ikiondoka patupu.

Michuano hiyo iliyoanza Agosti 1, 2026 na kumalizika Agosti 13, 2026, ilifanyika kwenye uwanja wa ndani wa New Amaan Complex kisiwani Unguja, huku ikishirikisha timu saba kati ya 13 zilizotarajiwa kushiriki.

Timu zilizoshiriki ni wenyeji Zanzibar, Kenya, Uganda, Tanzania, Zambia, Malawi na Botwsana, huku Cameroon, DR Congo, Rwanda, Burundi, Mauritius na Sudani Kusini zikishindwa kushiriki kutokana na sababu mbalimbali.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

SABABU ZANZIBAR KUFANYA VIBAYA

Licha ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, lakini haikufanya vizuri kama ilivyotarajiwa.

Kati ya mechi sita ilizocheza katika hatua ya makundi, timu ya Kabaddi Zanzibar ilifanikiwa kushinda tatu, huku zingine ikiambulia vipigo.

Matokeo ya mechi hizo yalikuwa kama ifuatavyo; Zanzibar 25-45 Uganda, Zanzibar 33-21 Malawi, Zanzibar 41-26 Zambia, Zanzibar 15-55 Kenya, Zanzibar 37-42 Tanzania, Zanzibar 33- 05 Botswana na Zanzibar 33-41 Tanzania.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, alisema sababu ya timu hiyo kufanya vibaya ni kwamba haikuwa na maandalizi mazuri, huku ikikosa sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali.

Alisema, hapo walipofikia ni jitihada za Shirikisho pekee, hivyo hawakuwa na nguvu za kushindana kwani wachezaji hawakufanikiwa hata kukaa kambi ya pamoja.

“Timu haikuwa na sapoti kutoka kwa wadau, tulikuwa tunaungaunga tu maana timu yetu haikuweza kukaa hata kambi, wachezaji walitokea nyumbani kucheza mechi,” alisema.

Alisema, kitu kingine timu ya Kabaddi ya Zanzibar ya wanaume haina uzoefu wa mashindano makubwa kama hayo ikilinganishwa na ya wanawake.

Alieleza kuwa, ikiwa timu haina mfumo mzuri wa fedha, ni ngumu sana kuwa na kiwango kizuri katika michezo yake ndio sababu ya kukosa hata nafasi ya tatu ya michuano hiyo.


TIMU ZILIZOKWAMA KUSHIRIKI

Kiongozi huyo alisema, timu ambazo hazikufanikiwa kushiriki zilishindwa kuwezeshwa na mashirikisho yao na upande wao hawakuwa na uwezo wa kuwasaidia makazi na huduma nyingine.

“Uwezeshwaji katika nchi zao ulikuwa hafifu ndio maana hawakuweza kushiriki na sisi hatukuwa na uwezo wa kuwakodia hoteli kwani kazi yetu ni kuwachukua wakifika na kuwapeleka walipopata hoteli ya kukaa,” alisema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MASHINDANO YALIVYOKUWA

Timu ya Kenya na Uganda ni miongoni mwa timu zilizokuwa na ushindani mkubwa tangu kuanza kwa michuano hiyo hadi kufikia hatua ya fainali.

Zanzibar na Tanzania Bara ziliishia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo huku Tanzania Bara ikimaliza ikiwa nafasi ya tatu.

Katika mashindano hayo, mchezaji Juma Sultani kutoka Tanzania Bara alibuka mshambuliaji bora, Gasta Tenywa wa Uganda akiwa mlizi bora, huku Samuel Wafula akiibuka kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Rais wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Abdalla Abeid Juma, alisema Zanzibar ni mwanachama mpya katika mchezo huo duniani na imeendelea kuongeza ushiriki wake katika mashindano ya kimataifa.

Alisema Zanzibar tayari imeshiriki mara nne katika mashindano ya dunia ya kabaddi kwa wanawake, hatua inayoonesha kuwa mchezo huo unaendelea kupata nafasi hapa nchini.

Abdalla anazipongeza nchi zilizoshiriki mashindano hayo yaliyofanyika Zanzibar kwa kuonyesha vipaji na ushindani mkubwa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Said Kassim Marine, aliipongeza kamati ya maandalizi kwa kazi kubwa iliyofanya kufanikisha mashindano hayo.

Said alisema kuandaa mashindano ya Afrika si jambo dogo, hivyo mafanikio ya mashindano hayo yanaonyesha juhudi na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuendeleza michezo Zanzibar.

Naye, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo katika kuhakikisha michezo mbalimbali inapata nafasi ya kukua na kuendelezwa Zanzibar.

Pembe alieleza kuwa, mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa Zanzibar yana umuhimu katika kukuza vipaji vya wanamichezo na kuongeza uzoefu wao wa kushindana katika viwango vya kimataifa.


AKU WATOA NENO LA SHUKRANI

Shirikisho la Kabaddi Afrika (AKU), nalo limetoa shukrani kwa washirika, wadau, vyama vya kitaifa na wachezaji wote walioshiriki na kuchangia kufanikisha mashindano ya AFCON Kabaddi 2026.

“Tunatoa shukrani za pekee kwa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar kwa maandalizi bora, uratibu na uendeshaji mzuri wa mashindano haya makubwa, kujitolea, dhamira na ukarimu wenu vimekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mashindano haya,” ilisema taarifa kutoka AKU.

Pia, AKU imevishukuru vyama vyote vya kitaifa vilivyoshiriki, pamoja na wachezaji, viongozi, makocha, waamuzi, wajitolea, washirika na wadau mbalimbali kwa kuungana kusherehekea na kuendeleza mchezo wa Kabaddi barani Afrika.

“Tunawashukuru nyote kwa kuwa sehemu muhimu ya AFCON Kabaddi 2026 na kwa kusaidia kufanya mashindano haya kuwa ya mafanikio na ya kukumbukwa. Kwa pamoja, tunaendelea kuimarisha, kukuza na kuunganisha mchezo wa Kabaddi barani Afrika,” ilisema taarifa hiyo.