Xabi hana jibu, kwa nini Chelsea inafunga mabao mengi mapema?
Muktasari:
- Wiki iliyopita, kikosi hicho kilikabiliana na Bournemouth kikiwa kimefunga mabao matatu ndani ya dakika tano za mwanzo katika mechi zake tano za kwanza za Ligi Kuu England, huku timu nyingine 19 kwa pamoja zilikuwa zimefunga mabao mawili tu katika kipindi hicho.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imeanza enzi za Xabi Alonso kwa kufunga idadi kubwa ya mabao katika dakika za mwanzo za mechi, lakini kwa nini timu hiyo huanza vizuri kiasi hicho, na kwa nini baadaye hushindwa kuendeleza kiwango hicho? Licha ya kufanya hivyo mara nyingi tayari, bado inashangaza kila mara Chelsea inaporudia kwa mtindo huo.
Wiki iliyopita, kikosi hicho kilikabiliana na Bournemouth kikiwa kimefunga mabao matatu ndani ya dakika tano za mwanzo katika mechi zake tano za kwanza za Ligi Kuu England, huku timu nyingine 19 kwa pamoja zilikuwa zimefunga mabao mawili tu katika kipindi hicho.
Hata hivyo, bado lilikuwa jambo la kushangaza kuona Chelsea ikiongeza idadi hiyo, hasa kutokana na namna ilivyofanya hivyo.
Kwanza, haikufunga bao moja tu ndani ya dakika tano za mwanzo wa mechi, bali mabao mawili. Pia, haikufanya hivyo ndani ya dakika tano pekee, bali tatu. Kupitia mabao ya Jordan Henderson na Morgan Rogers kabla saa haijaonyesha dakika 2:29, Chelsea iliongoza 2-0 ambayo ni rekodi ya tatu kuwahi kupatikana mapema zaidi katika historia ya ligi hiyo. Rekodi hiyo inafuatia mechi za Leicester dhidi ya Derby, Aprili 1998 na Luton dhidi ya Brighton, Januari 2024.
Kwa kuzingatia kuwa utawala wa Alonso ulianza kwa bao la Joao Pedro baada ya sekunde 31 katika mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Fulham, bao la Romeo Lavia dakika ya nne dhidi ya Brighton na la Rogers dakika ya pili dhidi ya Arsenal, wapinzani waliofuata wangeweza kujipanga kwa kuzingatia kasi ya kuanza kwa Chelsea. Hata hivyo, Chelsea ilifunga ndani ya dakika saba dhidi ya Hull City, kisha ikafunga mabao mawili ndani ya dakika tatu za mwanzo dhidi ya Bournemouth.
Tatizo kwa wapinzani wake ni kwamba hakuna mfumo maalumu wanaoweza kuufuata ili kuzuia hali hiyo. Chelsea haishambulii kwa namna moja maalumu katika hatua za mwanzo za mechi. Hakuna jambo moja au mtindo maalumu ambao wapinzani wake wa baadaye wanapaswa kuuangalia kama tahadhari.
Ni mara moja tu msimu huu ambapo Chelsea ilianza mechi ikiwa na dhamira ya wazi ya kuwarudisha wapinzani nyuma kwa kupiga mpira moja kwa moja kutoka kwenye mpira wa kuanza mchezo ili kupata wa kurushwa ndani ya eneo la mpinzani. Hiyo ilikuwa katika kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Brentford, mechi pekee ambayo Chelsea haikufunga bao la mapema, wala kufunga bao lolote.
Kocha wao anasisitiza kuwa hakuna mpango maalumu wa kuanza mechi kwa kasi, wala nia ya kuanza mchezo kwa kuzingatia kufunga bao mapema. “Sina uhusiano wowote na jambo hilo, kwa hiyo sina jibu. Sina maelezo, hivyo siwezi kujipa sifa,” anasema Alonso baada ya ushindi dhidi ya Bournemouth
ROGERS HAKUBALIANI
Kiungo wa Chelsea, Rongers anapinga akisema: “Nahusisha jambo hilo na maelekezo ya kocha kabla ya mechi,” alisema kiungo huyo baada ya kufunga dhidi ya Bournemouth, ikiwa ni bao lake la tatu alilofunga ndani ya dakika saba za mwanzo za mechi ya Ligi Kuu England.
“Anatuchochea na kutupa hamasa. Siku zote tunataka kuanza mchezo tukiwa na nguvu na kuchukua udhibiti. Jambo muhimu ni kuanza vizuri na kupata uongozi. Katika mechi nyingi, hasa tunapocheza nyumbani, tumekuwa tukishinda baada ya kutumia vizuri mabao ya mapema. Hiyo ni sifa nzuri ambayo tunahitaji kuendelea nayo,” anasema.
Huenda kocha Alonso mwenyewe hatambui kuwa anachangia hali hiyo, lakini maelezo ya Rogers yanaashiria kuwa maneno ya kocha kabla ya mechi yana athari kwa wachezaji. Pia, huenda wachezaji wanahisi kuwa na kasi ya ushindi na kujiamini.
Taarifa kutoka ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo zinaonyesha kuwa wachezaji wanaamini wanaweza kufunga bao la mapema, huku wakitania kuhusu nani atakayelifunga, badala ya kujiuliza kama timu itafunga bao kabisa.
TWENDE PAMOJA
Bila kujali sababu, jambo lililo wazi ni idadi kubwa ya mabao ya mapema na ufanisi wa Chelsea katika kutumia nafasi inazopata mwanzoni mwa mechi. Msimu huu, Chelsea imefunga mabao manne ndani ya dakika tatu za mwanzo wa mechi za Ligi Kuu England, huku timu nyingine 19 kwa pamoja zikiwa na mabao mawili pekee.
Mabao manne ya Chelsea katika kipindi hicho yametokana na mashuti matano tu yaliyopigwa, yakiwa na thamani ya mabao tarajiwa (xG) ya 0.71. Mabao mawili yaliyofungwa na timu nyingine zote yamekaribia kuendana kikamilifu na thamani ya mabao tarajiwa ya mashuti yao, ambayo ni xG 1.92.
Ndani ya dakika tano za mwanzo wa mechi, Chelsea imefunga mabao matano kutokana na xG 1.52. Kipindi kikiongezwa hadi dakika 15 za mwanzo, imefunga mabao saba kutokana na xG 2.28. Chelsea imevuka kwa kiasi kikubwa thamani ya mabao tarajiwa mapema kwa sababu karibu mabao yote hayo yametokana na nafasi ngumu kufunga.
Bao la Joao Pedro dhidi ya Fulham lilikuwa la kuvutia, akiuinua mpira juu ya kipa. Bao la Rogers dhidi ya Arsenal lilikuwa shuti la kuunganisha mpira hewani kutoka ukingoni mwa eneo la penalti, huku bao lake la kwanza dhidi ya Hull likiwa shuti zuri la chini kutoka kona ya eneo la penalti. Mabao yote mawili ya mapema dhidi ya Bournemouth mwishoni mwa wiki iliyopita yalipigwa kwa umbali mrefu, huku mastaa wengi wa wapinzani wakiwa kwenye njia ya mpira.
Huenda wachezaji wa Chelsea wanahisi kuwa mwanzoni mwa mechi wana uhuru zaidi wa kupiga mashuti ya mbali. Wanapata ujasiri wa kujaribu mambo ambayo huenda wasiyajaribu baadaye katika mchezo, kwa sababu shinikizo la kuhakikisha kila nafasi inazaa bao huwa bado halijawa kubwa. Hali hiyo, ikiunganishwa na kujiamini wanakopata kutoka kwa Alonso, huenda ikawa mchanganyiko wenye matokeo mazuri.
Ni wazi pia kuwa Chelsea ina wachezaji wengi wenye vipaji vya kushambulia, ambao wote wameanza msimu wakiwa katika viwango vizuri. Kwa hiyo, huenda ikawa ni bahati tu kwamba wanafanya vizuri kiasi hicho katika dakika za mwanzo za mechi.
Hata hivyo, rekodi yao inavutia bila shaka. Katika dakika 15 za mwanzo za mechi za Ligi Kuu England msimu huu, Chelsea ina tofauti ya mabao ya +7, ikiwa imefunga saba bila kuruhusu bao lolote. Hayo ni mabao matatu zaidi ya timu nyingine yoyote katika kipindi chochote cha dakika 15 za mchezo.
Manchester City ina tofauti ya mabao ya +4 kati ya dakika ya 75 na 90, huku Brighton ikiwa na +4 kati ya dakika ya 30 na 45. Nje ya kipindi hicho cha dakika 15 za mwanzo, Chelsea ina tofauti ya mabao ya -5.
Huo ni mwenendo wa kipekee, na ni vigumu kupata sababu ya tofauti hiyo. Kuna uwezekano wachezaji wa Chelsea wanachoka baada ya kuanza kwa kasi kubwa, huku timu hiyo pia ikidhoofika kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya wachezaji kadiri mechi zinavyoendelea.
Jambo lingine ni kwamba, kwa kuwa karibu kila mara Chelsea hupata bao la mapema, wapinzani wake hucheza sehemu kubwa ya mechi wakiwa nyuma kwa bao moja au mawili, hivyo hulazimika kushambulia zaidi.
Hali hiyo inaweza kuisha kadiri msimu unavyoendelea au wapinzani wanavyoanza kuzingatia zaidi namna ya kuizuia Chelsea katika dakika za mwanzo. Lakini kwa sasa, kikosi cha Alonso kiko kwenye njia nzuri ya kuvunja rekodi kadhaa za Ligi Kuu England zinazohusu mabao ya mapema.
Kwa mabao saba, Chelsea tayari imefikia zaidi ya theluthi moja ya rekodi ya mabao mengi zaidi yaliyofungwa ndani ya dakika 15 za mwanzo wa mechi za Ligi Kuu England. Rekodi hiyo ni mabao 19 yaliyofungwa na Man City 2018/19, licha ya Chelsea kucheza mechi sita tu tangu msimu huu uanze.
Mabao matano iliyofunga Chelsea ndani ya dakika tano za mwanzo yanaifanya kuvuka nusu ya njia ya kufikia rekodi ya msimu mzima, ambayo ni mabao tisa yaliyofungwa na Liverpool 2013/14. Kwa upande mwingine, mabao manne ndani ya dakika tatu za mwanzo yanaifanya Chelsea, kwa kushangaza, kuwa imebakiza mabao mawili tu kufikia rekodi ya msimu mzima, ambayo ni mabao sita yaliyofungwa na Man United 2010/11.
Jambo la kuzingatia ni kwamba timu mbili kati ya zilizoweka rekodi hizo, Man City 2018/19 na Man United 2010/11, zilishinda ubingwa wa ligi katika misimu hiyo. Timu nyingine, Liverpool 2013/14, ilikaribia sana kutwaa ubingwa. Hata hivyo, Chelsea inaonekana kuwa mbali sana na ushindani wa ubingwa msimu huu.
Sababu kubwa ni kwamba safu yake ya ulinzi imekuwa dhaifu sana, ikiruhusu mabao mengi zaidi ikilinganishwa na timu nyingine zote katika Ligi Kuu England msimu huu, ikiwa imeruhusu 13. Hakuna timu nyingine kati ya nane za juu kwenye msimamo wa ligi iliyofungwa zaidi ya mabao sita.