Prime
WAZEE WAKUVIZIA! Wakisogelea boksi lako, wanagusa moja mpira unaletwa kati

Muktasari:
- Kwenye soka la kisasa, kizazi hicho cha wachezaji hodari wa kupasia nyavu wamekuwa adimu kwa sababu mpira wa sasa umekuwa wa kiufundi zaidi kwa sababu makocha wamekuwa wakiwekeza nguvu zaidi kwenye kutengeneza mabao kuliko kuhangaika kusajili wafungaji tu (poachers). Waviziaji.
LONDON, ENGLAND: KITU kigumu kwenye soka ni kufunga bao. Hilo ni jambo gumu sana kwa wachezaji wengi. Lakini, kuna baadhi ya wachezaji suala la kufunga mabao walilifanya kuonekana kuwa jepesi hasa wale waliokuwa wakifahamika kama wawindaji ndani ya uwanja - wenyewe beki akijichanganya tu wanagusa mpira unawekwa kati.
Kwenye soka la kisasa, kizazi hicho cha wachezaji hodari wa kupasia nyavu wamekuwa adimu kwa sababu mpira wa sasa umekuwa wa kiufundi zaidi kwa sababu makocha wamekuwa wakiwekeza nguvu zaidi kwenye kutengeneza mabao kuliko kuhangaika kusajili wafungaji tu (poachers). Waviziaji.
Washambuliaji hao wa staili ya soka la zamani, wenyewe hawakuwa wakihangaika kujua kupiga chenga. Wenyewe walikuwa wanasubiri tu ndani ya boksi la mpinzani mpira uje, waguse kupasia nyavuni.
Hata hivyo, sio kila mchezaji alikuwa na uwezo wa kufunga kama waliokuwa nao washambuliaji hao wanaofahamika kama poachers. Wenyewe walikuwa hodari kukimbia kwa kuzingatia muvu na kujiweka kwenye maeneo hatari na mepesi kufunga.
Walikuwa na uwezo mkubwa wa kugusa kwa usahihi mpira wa kwanza, kwamba wanaweza kufunga kwa kugusa mpira mara moja au mbili, umekwisha.
Washambuliaji hao walikuwa wanaotea maeneo ya mpira kupita, wananusa uelekeo wa mpira kupita kwenye eneo la hatari. Kitu kama hicho kimezungumzwa mara nyingi, kwamba hakifundishwi, chenyewe ni kipaji cha asili. Kwa kifupi tu, washambuliaji wa aina hiyo wamekuwa wakipachikwa jina la ‘wapasia nyavu’, huku wengi wao hawakuwa na milii mikubwa.
Makala haya yanahusu washambuliaji ambao wenyewe hawakuwa wakihitaji kugusa mpira mara nyingi ndani ya boksi, wenyewe moja tu wanapasia nyavu, mpira unaletwa kati.

10. Ole Gunnar Solskjaer (mechi 529, mabao 282)
Ole Gunnar Solskjaer sehemu kubwa ya maisha yake kwenye kikosi cha Manchester United alikuwa akitokea benchini wakati huo chini ya Sir Alex Ferguson, ambapo alipachikwa jina maarufu la “super-sub”.
Straika huyo wa Norway hakuwa mchezaji mwenye kasi sana, wala mwenye nguvu, lakini alikuwa akijiweka kwenye maeneo sahihi kwa wakati sahihi. Kumruhusu aingie kwenye boksi lako, muda wowote anakuachia maumivu, ukiwauliza Bayern Munich watakuwa na majibu sahihi alichowafanya kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Nou Camp msimu wa 1998/99. Alichojua Solskjaer ni kupasia tu nyavuni.

9. Gary Lineker (mechi 573, mabao 283)
Kabla ya kuwa mtangazaji wa kipindi cha BBC Match of the Day, Gary Lineker alikuwa mpasia nyavuni mahiri wa staili ile ya waviziani wa ndani ya boksi kwenye miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90. Mwingereza hakutaka kabisa kujichoshwa nje ya boksi, ambapo yeye mabao yake mengi alikuwa akifunga ndani ya boksi, pale kwenye sita. Hakika, alikuwa mmoja wa mastraika mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye ligi kubwa ya England, huku Lineker akiwa mchezaji pekee ambaye alikuwa kinara wa mahao kwenye soka la England katika timu tatu tofauti- Leicester City, Everton na Tottenham Hotspur. Alitamba pia Barcelona, ambako alifunga hat-trick za ndani ya boksi dhidi ya Real Madrid.

8. David Trezeguet (mechi 559, mabao 273)
Watoto wa mwaka 2000 wanaweza wasilitambue hili jina la David Trezeguet. Huyo alikuwa straika wa Ufaransa, ambaye alikuwa akicheza soka kwa staili ya kizamani na kufunga mabao kwa staili hiyo hiyo ya kale. Hakuwa anaweza kukokota mpira kuwavuka mabeki watano wa timu pinzani au kupiga shuti akiwa nje ya boksi, yeye alichokuwa anafanya ni kuotea tu mpira ya krosi uelekeo wake, akivizia kwenye boksi na kupasia mpira nyavuni. Trezeguet alikuwa mahiri sana wa kuokota mpira iliyokuwa inazagaazagaa ndani ya boksi. Kwa namna alivyokuwa anajipanga na uwezo wake wa kupasia mpira nyavuni kwa kugusa mara moja tu, ilikuwa ikiwafanya mabeki wengi kuchukia kucheza dhidi yake, akiwatesa alipokuwa Monaco, Juventus na timu ya taifa ya Ufaransa, Les Bleus.

7. Gerd Muller (mechi 728, mabao 656)
Alipachikwa jina la “Der Bomber,” Gerd Muller alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufunga mabao kwenye nafasi finyu sana na alikuwa mwepesi wa kuwahi mpira ndani ya boksi kuliko mabeki wa timu pinzani. Rekodi zake za kufunga kwenye kikosi cha Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani zinajieleza zenyewe. Katika misimu yake 15 kwenye kikosi cha Bayern Munich, Muller alifunga mabao 570 katika mechi 613 alizocheza kwenye michuano yote. Hilo lilimfanya awe na wastani wa bao moja kwa kila mechi alipokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani Magharibi, alipofunga mabao 68 katika mechi 62. Mjerumani huyo mkali wa kupasia nyavuni ni mmoja kati ya wachezaji tisa ambao walishinda Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ballon d’Or.

6. Alan Shearer (mechi 734, mabao 379)
Kinara wa mabao wa muda wote kwenye Ligi Kuu England. Alan Shearer, hakuwa tu straika wa nguvu, bali alikuwa fundi wa kumalizia mipira ile ya kugusa mara moja tu unaweka nyavuni na hakika alikuwa matata alipokuwa ndani ya boksi. Shearer nguvu yake kubwa ilikuwa kwenye mipira ya vichwa, lakini mabao yake 260 anayotamba nayo kwenye Ligi Kuu England, alifunga ndani ya boksi. Sawa, kuna mabao ya mashuti ya mbali alifunga pia, lakini sehemu kubwa ya mabao yake aliyofunga Namba 9 huyo kwenye Ligi Kuu England ni yale ya ndani ya boksi. Kwa sababu hakuchezea timu iliyokuwa ikitawala soka la England, straika huyo alifanikiwa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England mara moja tu, alipokuwa Blackburn Rovers msimu wa 1994/95.

5. Hugo Sanchez (mechi 821, mabao 484)
Hugo Sanchez anatambulika kama mwanasoka mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye soka la Mexico. Staa huyo alikuwa kiboko kwa kumalizia mpira kwenye nyavu, licha ya kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na video zake zinazomwonyesha alivyokuwa mahiri kufunga mabao ya tick-tack. Staa huyo alikuwa hatari sana ndani ya boksi, ambapo kwenye La Liga alifunga mabao 234. Staa huyo wa Mexico alikuwa na kasi sana ndani ya boksi, mikimbio mizuri pamoja na kujiweka kwenye maeneo ambayo mabeki walikuwa wakidhani hana madhara, lakini mpira ulipomfikia tu, aliwachia maumivu. Licha ya kwamba alikuwa na mwili mdogo, lakini Sanchez alikuwa matata pia kwa kufunga mabao ya vichwa mbele ya mabeki warefu na wenye miili mikubwa.

4. Filippo Inzaghi (mechi 624, mabao 288)
Kuna mtu anaitwa Filippo Inzaghi. Hakuwa na kasi, wala ufundi mwingi wa kupiga chenga mabeki au kupiga pasi, lakini straika huyo Mtaliano alikuwa mnyama ndani ya boksi. Kitu cha ziada kuhusu straika huyo, alikuwa mjanja sana wa kukwepa mtego wa kuotea, ambapo alikuwa na mikimbio yake ya nyuma ya mstari wa mabeki. Jambo hilo lilimfanya awe mmoja wa mastraika matata sana kwenye kupasia mpira nyavuni, ambapo alifunga mabao 288 katika mechi 624 alizocheza, huku akiifungia Italia mara 25 katika mechi 57. Staili yake hiyo ya uchezaji ya kizamani kwenye kuvizia tu ndani ya boksi, imemfanya ashinde Serie A mara tatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na Kombe la Dunia 2006.

3. Ruud van Nistelrooy (mechi 592, mabao 349)
Bila ubishi moja ya wamaliziaji bora kabisa kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England alikuwa Ruud van Nistelrooy, ambaye mara chache sana alifunga mabao yake nje ya boksi. Kwa nyakati zake alizotamba kwenye kikosi cha Manchester United na Real Madrid, alitamba na ile staili yake ya kutoka pembeni na kuingia ndani, mipira inayozagaazagaa na ile ya kugusa tu nyavuni. Alikuwa na uwezo wa kutambua mikimbio ya mabeki wa timu pinzani, hivyo alitumia hilo kuwazidi ujanja ndani ya penalti boksi. Wakati alipokuwa Man United, Mdachi huyo mara tatu tofauti alimaliza msimu akiwa kinara wa mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akishika namba sita kuwa kinara wa muda wote wa mabao kwenye michuano ya Ulaya, mabao 56.

2. Javier Hernandez (mechi 531, mabao 198)
Javier Hernandez, maarufu kwa jina la ‘Chicharito’, alijijengea umaarufu mkubwa sana kwa kuwa mahiri ndani ya boksi kwenye ligi kubwa alizocheza Ulaya. Alikuwa mkali wa kufunga mabao ya kugusa mara moja tu, nyavuni. Alikuwa na uwezo wa kuzibadili hata zile nusu nafasi kuwa nafasi kamili na alikuwa toleo la mwisho la washambuliaji wa staili ya kuvizia ndani ya boksi. Iwe kwenye kikosi cha Manchester United, Bayer Leverkusen au kwenye timu ya taifa ya Mexico, mara zote Chicharito alikuwa akijikuta akimalizia mipira ambao ilikuwa yakibabatiza mabeki, kupanguliwa na kipa au kugonga mwamba na zile krosi za chinichini. Alikuwa mahiri pia kwa mipira ya kichwa na staili yake ya uchezaji ilimfanya kocha wa Man United kwa wakati huo, Sir Alex Ferguson kumlinganisha na Ole Gunnar Solskjaer.

- Miroslav Klose (mechi 667, mabao 258)
Miroslav Klose huyu sasa alikuwa kiboko kwenye orodha ya washambuliaji wote waliokuwa waviziaji mahiri ndani ya boksi la timu pinzani. Ilikuwa ikimsahau sekunde tu, ameshakuletea maumivu. Mjerumani huyo ni gwiji kwenye Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao 16 ya fainali hizo, akivunja rekodi. Ndiye kinara wa mabao wa Ujerumani, alikuwa mnyama mkali ndani ya eneo la penalti. Wakati akiwa si mchezaji mwenye mbwembwe nyingi, Klose alikuwa bora kwenye kuwahi mipira ya kubabatiza inayorudi uwanjani, krosi na yale mashambulizi ya kutokea pembeni na muda wote alikuwa akijiweka kwenye nafasi zinazompa urahisi kufunga. Klose hakuwa na kasi, lakini alikuwa na mikimbio ya kijanja ndani ya uwanja iliyokuwa ikiwapoteza mabeki wa timu pinzani na kufunga kirahisi ndani ya boksi.