Watkins, Sesko nani anatosha Man United?
Muktasari:
- Man United bado inataka kuongeza straika mpya kwenye kikosi chake na sasa, wakati dirisha hili likiendelea kuwa wazi, majina mawili makubwa yanayotajwa ni Ollie Watkins na Benjamin Sesko.
LONDON, ENGLAND: OLLIE Watkins au Benjamin Sesko? Nani ataweza kufiti vyema kwenye fowadi ya Manchester United? Swali gumu linapokuja suala la ndani ya uwanja, lakini linajibika kiwepesi kwenye karatasi.
Man United bado inataka kuongeza straika mpya kwenye kikosi chake na sasa, wakati dirisha hili likiendelea kuwa wazi, majina mawili makubwa yanayotajwa ni Ollie Watkins na Benjamin Sesko.
Baada ya kuwaongeza kwenye kikosi mastaa Matheus Cunha kutoka Wolves na Bryan Mbeumo kutoka Brentford, wachezaji ambao wote walikuwa na rekodi nzuri ya kufunga msimu uliopita, Man United bado inataka kuboresha safu yake ya ushambuliaji kwa ajili ya msimu mpya.
Man United haikuwa na wastani mzuri wa mabao yake kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ilifunga mara 42 na kuthibitisha haikuwa na wakati mzuri kabisa mbele ya magoli ya wapinzani.
Washambuliaji wake, Joshua Zirkzee na Rasmus Hojlund walikuwa butu mbele ya goli na wa kwanza alifunga mara tatu na wa pili mara nne kwenye mechi walizocheza kwenye ligi.
Kocha Ruben Amorim atahitaji kufanya vizuri, hasa katika kipindi ambacho utakuwa msimu wake wa kwanza mzima kwenye timu hiyo, hivyo atakuwa na kazi ya kusajili straika mpya kuja kufanya shughuli ya kutikisa nyavu.
Watkins vs Sesko
Watkins ameshaonyesha kiwango bora kwenye Ligi Kuu England kwa misimu ya hivi karibuni na amefunga mabao 75 katika mechi 184 alizocheza kwenye ligi, huku akiasisti 36 pia.
Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 29, amehusika kwenye mabao 20+ kwa maana ya kufunga au kuasisti katika misimu mitatu iliyopita kwenye Ligi Kuu England, huku kiwango chake bora zaidi kilikuwa kwenye msimu wa 2023-24, alipofunga mabao 19 na kuasisti 15 na alizidiwa na Cole Palmer tu katika ubora huo wa uwanjani.
Watkins ni straika hasa hasa kutokana na uwezo wake wa kunusa nafasi za mabao anapokuwa ndani ya boksi la mpinzani, huku akiwa na wastani wa kugusa mpira mara sita au zaidi ndani ya boksi la mpinzani ndani ya dakika 90, huku akiwa na wastani wa kufunga bao 0.6 kwa dakika 90 akiwa nje ya boksi.
Sesko, kwa upande wake, ana wastani wa kugusa mpira mara tatu au zaidi ndani ya boksi la mpinzani ndani ya dakika 90, huku akiwa na wastani wa kufunga mabao 0.5 kwa dakika tisa, huku 0.4 ikiwa ndani ya boksi na 0.2 nje ya boksi.
Straika huyo mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akipenda sana kupiga mashuti ya mbali na amekuwa na shabaha kubwa ya kulenga goli.
Namna anavyojiamini, ubora na kiwango matata za kucheza mipira ya juu, kutokana na kuwa na kimo cha fupi 6 na inchi 5, jambo linalomfanya alinganishwe na straika wa zamani wa Man United, Zlatan Ibrahimovic.
Nani anafiti Man United: Watkins au Sesko?
Watkins yupo kwenye mfumo unaotumiwa na Man United kwenye usajili wao wa dirisha hili la kunasa mastaa ambao tayari wameshaonyesha kiwango cha kutosha kwenye Ligi Kuu England, wakiamini wataenda kufanya kitu kikubwa kwenye kikosi chao.
Staa huyo wa kimataifa wa England alifanya vizuri pia kwenye ligi msimu uliopita, kwenye ishu ya mabao kwa mechi, kama ilivyokuwa kwa mastaa Cunha na Mbeumo.
Watkins pia ni mshambuliaji anayependa kukimbia, kitu ambacho Amorim anakihitaji ili kuongeza kasi kwenye eneo la mbele la timu yake na ndiyo maana amefanya usajili wa mastaa kama Cunha na Mbeumo.
Hata hivyo, kwa umri wa miaka 29, hiyo ina maana Watkins utakuwa usajili wa mipango ya muda mfupi, haipi timu nafasi ya kumuuza tena ili kupata pesa, hivyo ukimsajili ina maana atakwenda kumaliza soka lake akiwa kwenye kikosi chao, la akiondoka basi haitakuwa kwa faida.
Kwa upande mwingine, Sesko umri wake ni miaka 22 tu na kama anavyouzwa kwa pesa nyingi kwa sasa, Man United pia itakuwa na nafasi ya kumtumia kwa muda mrefu na inaweza kumuuza kwa faida endapo kama atakuwa bora zaidi.
Sesko alikuwa na kiwango bora pia kwenye Bundesliga msimu uliopita na kwa msimu wa 2023/24 alikuwa na wastani wa +6.3 wa bao kwa mechi na msimu uliopita alikuwa na wastani wa +3.0.
Mastraika hao wote wanaweza kumpa viwango tofauti kocha Amorim na Sesko ni balaa zaidi nje ya boksi kutokana na kuwa na ufundi mwingi, wakati Watkins ni mbwa mwitu ndani ya boksi, ambaye atakufungia mabao ya kutosha.
Faida nyingine ya Sesko kwamba anakupa matumaini ya kuja kuwa straika bora duniani kitu ambacho kitaipa faida kubwa Man United endapo kama itamsajili na kuvumilia naye kikosini kwa muda mrefu.
Kwa maana hiyo, kwenye karatasi, Watkins anaweza kuonekana kama ni chaguo zuri kwa Man United kutokana na ameshaonyesha kitu kwenye Ligi Kuu England, mtu ambaye Amorim anamhitaji ili kurekebisha mambo kwa haraka.