Kuna mmoja atakimbia Uwanja wa Uhuru
Muktasari:
- Na pasipo kuchelewa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imetutangazia kwamba timu mbili kubwa nchini za Simba na Yanga zitautumia uwanja huo kwa ajili ya mechi zao za nyumbani za mashindano tofauti msimu ujao.
HATIMAYE Uwanja wa Uhuru uliopo pale kata ya Chang’ombe mkoa wa Dar es Salaam umekamilika rasmi na sasa upo tayari kutumika kwa mechi mbalimbali za soka.
Na pasipo kuchelewa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imetutangazia kwamba timu mbili kubwa nchini za Simba na Yanga zitautumia uwanja huo kwa ajili ya mechi zao za nyumbani za mashindano tofauti msimu ujao.
Hii kwa sababu Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao umekuwa ukitumiwa mara kwa mara na timu hizo, upo katika ujenzi wa kuuandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambazo zitafanyika hapa nchini kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, hata mechi za watani wa jadi baina ya timu hizo, ‘Kariakoo Dabi’ zote mbili kwa msimu ujao zitapigwa katika uwanja huohuo wa Uhuru ambao miaka mingi nyuma ulijulikana kama Uwanja wa Taifa.
Hata hivyo kitu rahisi ambacho kijiwe kinaweza kukitabiri ni kwamba timu moja kati ya hizo mbili, haitomaliza msimu ikiwa inatumia Uwanja huo wa Uhuru kwa mechi zake za nyumbani.
Tena inawezekana hata ikawa ndani ya mwaka huu, tukashuhudia ama Yanga au Simba ikaondoka katika Uwanja wa Uhuru na kuhamishia majeshi kwingine badala ya kubakia katika uwanja huo.
Hii ni kwa sababu klabu hizo mbili huwa na utamaduni wa kukwepana katika matumizi ya uwanja hasa pale inapotokea mojawapo imeshindwa kufanya vizuri katika mechi moja au zaidi halafu upande mwingine mambo yakanyooka.
Mfano msimu wa 2024-2025, Simba iliondoka katika Uwanja wa Azam Complex ambao ilikuwa ikiitumia pamoja na Yanga na ikaelekea katika Uwanja wa KMC Complex lakini baadaye ikafuatwa na watani wao.
Baada ya Yanga kuwafuata hapo, Simba muda mfupi baadaye wakaondoka na kwenda Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, kisha ikarudi na kumaliza msimu wa 2025-2026.