Baleba njia yake Man United yahitaji subira
Muktasari:
- Jeraha lilichelewesha mwanzo wa safari yake ndani ya United na kumkosesha nafasi ya kuonyesha mara moja kwa mashabiki sababu iliyoufanya uongozi wa klabu hiyo kupambana kwa nguvu kumsajili.
LONDON, ENGLAND; KIUNGO Carlos Baleba ametumia miaka mingi akiota siku ambayo angevaa jezi ya Manchester United na kushuka kwenye Uwanja wa Old Trafford, lakini baada ya kukamilisha uhamisho wake mkubwa kwenda klabuni hapo, kiungo huyo wa Cameroon amelazimika kuvumilia jambo gumu zaidi la kusubiri.
Jeraha lilichelewesha mwanzo wa safari yake ndani ya United na kumkosesha nafasi ya kuonyesha mara moja kwa mashabiki sababu iliyoufanya uongozi wa klabu hiyo kupambana kwa nguvu kumsajili.
Hata hivyo, nyuma ya pazia, Baleba ameanza kuzoea maisha yake mapya kwa msaada wa watu wake wa karibu wanaohakikisha anabaki na utulivu na kutokubali mafanikio yambadilishe.
Kiungo huyo wa zamani wa Brighton ameendelea kutumia mfumo uleule wa maisha uliomsaidia kufanya vizuri wakati akiwa kusini mwa England.
Mpishi wake binafsi bado ni sehemu ya timu yake, huku dada yake akiishi naye na meneja wake wa muda mrefu, Patrick, akiendelea kuwa mtu muhimu katika maisha yake.
Patrick ndiye aliyemsaidia Baleba kujiunga na Lille akiwa kijana, kabla ya kusimamia uhamisho wake kwenda Brighton na baadaye kuwa naye katika safari ndefu iliyomfikisha Old Trafford.
Mtandao huo wa watu wa karibu umemsaidia Baleba, 22, kupunguza presha na msongo wa mawazo ya kufika katika klabu aliyoiota kwa muda mrefu huku akiwa hawezi kuanza kucheza mara moja kutokana na jeraha.
Kwa bahati nzuri, jeraha hilo halionekani kuwa kubwa na kocha wa United, Michael Carrick, ameashiria kuwa Baleba anaweza kuwa tayari kucheza mechi yake ya kwanza baada ya mapumziko ya kalenda ya kimataifa.
Carrick alisema: “Atarudi na kuwa sehemu ya kikosi katika kipindi cha wiki moja hivi ijayo, hivyo baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa anapaswa kuwa katika hali nzuri.
“Carlos alikuja akiwa ameumia, lakini anatamani sana kutoka uwanjani, kuwa sehemu ya kikosi na kufanya mazoezi kikamilifu na wenzake.
“Nilishasema awali kuwa ni mchezaji mwenye ubora, ndiyo maana tulimsajili.
“Pia, anaendana vizuri na mahitaji ya safu yetu ya kiungo.”
Safari ya Baleba kwenda Old Trafford haijahusisha soka pekee. Akiwa Lille, alipoteza mama yake katika tukio lililomuumiza sana, jambo ambalo amewahi kueleza kuwa lilichangia kumjenga kuwa mtu alivyo sasa.
Baba yake bado yupo Cameroon ambako anafanya kazi ya ukocha, lakini tayari amefanya safari mbili kwenda Manchester tangu mwanawe alipohamia United msimu huu wa kiangazi.
Hata hivyo, hana mpango wa kuhamia England moja kwa moja. Familia imeamua kuendelea na mfumo uliomsaidia Baleba alipokuwa Brighton kwa kuwa karibu naye wakati anapowahitaji, huku wakimpa nafasi ya kujenga maisha yake kwa kujitegemea.
Msaada wa Baleba hauishii kwa familia yake pekee. Kocha wa Cameroon, David Pagou pia ameendelea kuwasiliana mara kwa mara na kiungo huyo wakati akipitia hatua hii kubwa ya maisha yake ya soka.
Pagou pia aliamua kutomjumuisha Baleba katika kikosi cha Cameroon kwa mechi za hivi karibuni za kimataifa, kwa sehemu kutokana na jeraha lake na pia kumpa muda muhimu wa kuzoea maisha mapya Manchester.
“Nimekuwa nikiwasiliana na Carlos siku zote, lakini siku hizi zaidi kwa sababu tunataka afike kiwango cha juu kabisa.
“Sikumuita kwenye kikosi hiki hasa kwa sababu ameumia, pia tunataka achukue muda wake na kuzoea vizuri.
“Amekuwa akilitamani nafasi hii, lakini nilimwambia njia ya kufanikiwa ni kujikita kwenye kazi, kufanya kazi kwa bidii na kuwasikiliza makocha wako.
“Tayari una kipaji, hivyo usikubali kelele za nje zikuvuruge na utafanikiwa huko,” alisema Pagou.
Nchini Cameroon, Baleba anachukuliwa na wengi kuwa mtoto aliyebarikiwa, huku safari yake kutoka Lille hadi Brighton na sasa Manchester United ikiendelea kuwa simulizi ya kijana anayesubiri nafasi yake ya kung'ara Old Trafford.