Ushindani, majeraha yanavyomuweka mtegoni Sopu Azam FC
Muktasari:
- Mkataba wa awali wa nyota huyo aliyejiunga na Azam FC, Julai 4, 2022 akitokea Coastal Union ulikuwa unafikia mwishoni mwa msimu wa 2024-2025, japo tangu ameongezewa mmoj, amekumbwa na majeraha ya mara kwa mara yanayomweka pia hatarini.
OKTOBA 31, 2024, uongozi wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC ulimuongezea mkataba wa mwaka mmoja kiungo nyota mshambuliaji wa timu hiyo, Abdul Suleiman ‘Sopu’ utakaomweka ndani ya kikosi hicho hadi mwisho mwa msimu wa 2025-2026.
Mkataba wa awali wa nyota huyo aliyejiunga na Azam FC, Julai 4, 2022 akitokea Coastal Union ulikuwa unafikia mwishoni mwa msimu wa 2024-2025, japo tangu ameongezewa mmoj, amekumbwa na majeraha ya mara kwa mara yanayomweka pia hatarini.
Sopu aliziingiza vitani miamba ya Kariakoo kwa maana ya Simba na Yanga, ingawa ni Azam iliyoshinda vita hiyo, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ wakati huo anaichezea hususani msimu wake wa 2021-2022.
Msimu huo wa 2021-2022, Sopu akiichezea Coastal Union, alifunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 28, kati ya 30, sawa na dakika 2451, huku akiiwezesha timu hiyo kufika fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la (FA).
Baada ya msimu huo bora, Sopu akajiunga rasmi na Azam, Julai 4, 2022, ambapo msimu wake wa kwanza wa 2022-2023, akiwa na kikosi hicho, aliendelea kufanya vizuri pia, baada ya kiungo huyo mshambuliaji kufunga mabao yake sita ya Ligi Kuu Bara.
Msimu huo ndio uliokuwa bora kwake akiichezea Azam katika kipindi cha misimu minne anayocheza hadi sasa, kwani msimu wa 2023-2024, ulikuwa ni mgumu zaidi kikosini, baada ya kiungo huyo kumaliza na bao moja tu la Ligi Kuu na kikosi hicho.
Sopu alifunga bao hilo dakika ya 29, dhidi ya JKT Tanzania, ambapo Azam ilishinda mabao 2-0, huku lingine likifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 90, mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Mei 21, 2024.
Msimu wa 2024-2025, nyota huyo akaja kwa kasi na kuhusika katika mabao saba ya Ligi Kuu Bara akiwa na timu hiyo, baada ya kufunga matatu na kuasisti manne, ingawa, msimu huu wa 2025-2026, ambao ni wa mwisho umekuwa ni mgumu kikosini humo.
REKODI INAYOISHI
Nyota huyu anashikilia rekodi tamu ya mchezaji pekee aliyefunga mabao matatu yaani ‘Hat-Trick’ katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la (FA) msimu wa 2021-2022, wakati huo akikichezea kikosi cha Coastal Union kutoka mjini Tanga.
Msimu huo wa 2021-2022, Sopu aliyafunga mabao hayo katika mechi ya fainali ya michuano hiyo dhidi ya Yanga, iliyopigwa Julai 2, 2022, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha na kuisha kwa Coastal Union kuchapwa kwa penalti 4-1.
Mechi hiyo iliisha kwa penalti 4-1 na Yanga kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya sare ya mabao 3-3, katika dakika 120, ambapo Sopu alifunga mabao hayo dakika ya 11, 88 na 98, hivyo, kuweka rekodi tamu inayoendelea kuishi hadi sasa.
Mabao ya Yanga katika mechi hiyo, yalifungwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayeichezea Azam kwa sasa dakika ya 57, Heritier Makambo aliye Namungo akafunga dakika 82 na Denis Nkane anayecheza TRA United kwa mkopo akafunga dakika ya 113.
Katika penalti hizo, Yanga ilifunga zote nne kupitia kwa Yannick Bangala, Heritier Makambo, Dickson Job na Khalid Aucho, huku Coastal United, ikipoteza mbili na kufunga moja tu ya aliyekuwa pia kiungo wa kikosi hicho, Mnigeria Victor Akpan.
KUTUPIA USIPIME
Licha tu ya kuandamwa na majeraha, ila Sopu, anashikilia rekodi bora ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, tangu iliporejea msimu wa 2015-2016, baada ya kutofanyika miaka 13, mfululizo kufuatia mara ya mwisho kufanyika mwaka 2002.
Rekodi bora anayoishikilia kiungo huyo mshambuliaji, ni ya kufunga mabao mengi katika Michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, aliyoiweka msimu wa 2021-2022, alipofunga mabao tisa, akiichezea Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ ya mjini, Tanga.
Nyota mwingine aliyefunga idadi sawa na hiyo ya Sopu, alikuwa ni mshambuliaji, Omari Yassin wa Panama FC aliyefunga pia mabao tisa msimu wa 2019-2020, ila, kuanzia hapo hadi leo hii hakuna mchezaji aliyefikisha hata mabao nane kwa msimu.
Msimu wa kwanza wa 2015-2016, wakati mashindano hayo yanarejea, mfungaji bora alikuwa ni Hamis Kiiza ‘Diego’, aliyefunga mabao matano akiichezea Simba, ingawa, idadi hiyo ilikuwa sawa na ya aliyekuwa mshambuliaji wa Ndanda FC, Atupele Green.
Kwa msimu wa 2016-2017, aliibuka mfungaji bora, Mzambia Obrey Chirwa akiwa Yanga aliyefunga mabao matano, ambaye msimu wa 2025-2026, nyota huyo ndiye kinara wa ufungaji katika Ligi ya Championship, baada ya kuifungia Kagera Sugar mabao 14.
Msimu uliofuatia wa 2017-2018 ulishuhudia Habibu Kyombo aliyekuwa akiichezea Mbao FC akimaliza kinara na mabao sita, huku msimu wa 2018-2019 ukiwa mgumu kwa washambuliaji, baada ya Seif Karihe kufunga mabao manne tu akiwa na Lipuli FC.
Karihe anayecheza kwa sasa Mashujaa FC, msimu huo wa 2018-2019, alifunga idadi sawa ya mabao na waliokuwa washambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo anayeichezea Namungo FC na Amissi Tambwe, ambaye ni meneja wa timu ya Singida Black Stars.
Baada ya hapo, msimu wa 2019-2020, Omari Yassin wa Panama akafunga mabao tisa, huku msimu wa 2020-2021, Reliants Lusajo akiwa na Namungo FC akaifungia mabao manne, kisha msimu wa 2021-2022, Sopu akafunga mabao tisa akiichezea Coastal Union.
Msimu wa 2022-2023, aliyekuwa nyota wa Ihefu kwa sasa Singida Black Stars, Andrew Simchimba, anayecheza Mtibwa Sugar kwa mkopo, alionyesha kiwango bora cha kuvutia, baada ya kumaliza akiwa mfungaji wa Michuano ya CRDB kwa kufunga mabao saba.
Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, anayeuguza majeraha kwa sasa, msimu wa 2023-2024, aliibuka mfungaji bora, baada ya kufunga mabao matano na kuipa taji timu hiyo, ikiwa ni idadi sawa pia ya mabao na nyota wa JKT Tanzania, Edward Songo.
Msimu uliopita wa 2024-2025, ambao Yanga ilitwaa ubingwa huo kwa mara ya nne mfululizo, mfungaji bora alikua ni nyota wa kikosi cha maafande wa JKT Tanzania, kilichoishia hatua ya nusu fainali, Mohamed Bakari, aliyefunga mabao yake matano.
USHINDANI WA NAMBA
Miongoni mwa vitu vinavyomtesa nyota huyo kwa sasa, ni kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha mbalimbali ambayo yanamkabili, huku wachezaji wanaocheza nafasi yake ndani ya kikosi hicho wakifanya vizuri na kutishia mustakabali wake.
Miongoni mwa nyota hao ni Idd Seleman ‘Nado’, ambaye amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2025-2026, huku Zidane Sereri, mwenye mawili na Nassor Saadun, aliyerejea akitokea majeruhi, wakiendelea kufanya vizuri kikosini.
Mnigeria Abel Abah, aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo la Januari 2026, akitokea KF Tirana ya Albania, akichezea pia FK Metalac ya Serbia, ni ingizo jipya linalotishia nafasi ya Sopu, kikosini, chini ya Kocha, Mkongomani Florent Ibenge.
Nyota mwingine anayefanya vizuri ni winga, Mzee Hassan Mzee ‘Aziz KI’ aliyesajiliwa pia katika dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM FC ya Zanzibar akizidisha ushindani wa nafasi na wengine kikosini.
Licha ya rekodi bora ya nyota huyo, ila ushindani wa nafasi ndani ya kikosi hicho cha Azam na mkataba wake kufikia pia mwisho mwa msimu huu, kunamweka katika wakati mgumu, ikiwa uongozi wa timu hiyo utampa mkataba mpya au wataachana naye.