Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unaijua Bungay na ma-Bungay wanaotaka tamasha la Bungay?

Muktasari:

  • Wengi wa watu wanaoshinikiza kufanyika kwa tukio kama hilo la kihistoria ni wanachama wa Klabu ya Bungay Town ambayo hivi sasa inashiriki ligi ya jimbo ya Norfolk/Suffolk.

MASHABIKI wa kandanda wa mji mdogo wa Bungay ambao upo kilomita 150 kutoka London karibu na mji wa Ipswich, wameanzisha kampeni ya kurudiwa kwa kioja kilichoshuhudiwa 2016 na kuahidi kuchangia kwa hali na mali ili tukio kama lile la miaka 10 iliyopita lifanyike tena.

Wengi wa watu wanaoshinikiza kufanyika kwa tukio kama hilo la kihistoria ni wanachama wa Klabu ya Bungay Town ambayo hivi sasa inashiriki ligi ya jimbo ya Norfolk/Suffolk.

Julai 16, 2016, ulimwengu wa mchezo wa kandanda ulishuhudia mkasa wa aina yake uliofanyika Uingereza na kuacha kumbukumbu isiyosahaulika ya mchezo ambao wachezaji wote 22 waliokuwepo uwanjani, makocha, madaktari wa timu, waamuzi, wasaidizi, wachua misuli na watoto waliokuwa pembeni kuokota mpira walikuwa watu wenye jina moja, na idadi ya watu hao walioshiriki mchezo huo kwa njia moja au nyingine ilikuwa 70. Jina hilo ni Bungay.

Safari hii mashabiki wanataka hata watazamaji watakaokaa jukwaa kuu la Uwanja wa Maltings Meadow uliopo katika kitongoji cha Ditchingham, nje ya mji wa Bungay wawe na jina la Bungay. Viongozi wa Chama cha Kandanda cha Southampton wanadai kwamba wanalifikiria ombi hilo  ambalo utekelezaji wake ni mgumu na gharama zake ni kubwa.

Mchezo wa 2016 ulifanyika katika huo mji wa Bungay, uliopo katika Jimbo la Suffolk, ambao una wakazi wapatao 6,000. Timu zote mbili zilizoshiriki katika mchezo huo ziliitwa Bungay. Wachezaji wanaume na wanawake, wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 40 walitoka Uingereza, New Zealand na Australia, wote wakiwa na jina la Bungay ambalo liliandikwa katika sare zao.

Vilevile, wachezaji wote waliandikwa mgongoni majina yao, nalo ni jina moja tu—Bungay. Hata hivyo, sare za wachezaji zilikuwa za rangi tofauti, lakini nembo za sare za timu zote mbili pia zilikuwa moja, nayo ni ya mtoto wa miaka minane aitwaye Bungay ambaye alikuwa anatibiwa na Dk Elizabeth Bungay.

Jina hilo la Bungay ni miongoni mwa majina ambayo siyo maarufu duniani, na baadhi ya watu wenye asili ya jina hilo wanafanya kila juhudi lisipotee, na kufanyika kwa mchezo wa mwaka 2016 ilikuwa moja ya juhudi za kulilinda. Katika sensa iliyofanyika Uingereza miaka 25 iliyopita iligunduliwa kuwepo watu 455 wanaoitwa Bungay, kama 12 kwa kila watu milioni moja wa nchi hiyo.

Wazo la kuwa na mchezo huo lilitokana na jamaa aitwaye Shaun Cole, aliyekuwa mjumbe wa kamati ya Klabu ya Bungay Town, kuamua kutafuta njia za kuimarisha klabu hiyo ambayo waumini wake ni wa Kanisa la Anglikana.

Alichukua miezi kadhaa kuwatafuta watu wanaoitwa Bungay, na miongoni mwa aliokutana nao ni jamaa aliyekuwa anaongoza kampuni moja aitwaye Bill Bungay, na katika mazungumzo yao walikubaliana kuwatafuta watu wengi wanaoitwa Bungay ili kwenda kucheza kandanda katika mji mdogo wa Bungay.

Katika msako huo wa majina ya watu wanaoitwa Bungay walipata familia 68 ambazo baadhi zilikubali kuwatafuta watu zaidi wanaoitwa Bungay. Miongoni mwa watu waliopatikana ni dereva mstaafu wa lori, Chris ‘Tiffer’ Bungay, 57, wa Queensland, Australia, ambaye alikubali kwenda Uingereza kucheza kandanda la tamasha la watu wa jamii ya Bungay.

Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuwatafuta waamuzi wenye sifa ya kuchezesha kandanda, na walifanikiwa kumpata John Bungay, 61, kutoka Hampshire, Uingereza, ambaye alikwenda na watoto wake Andrew, 37, na Graeme, 34. Matokeo ya mchezo ule yalikuwa sare ya mabao 6-6. Matokeo yale yalielezwa kuwa ndiyo sahihi kwa mchezo ule, kwa vile jina la Bungay pia lina herufi sita, na hivyo kila sita za matokeo zilikuwa zawadi za timu moja kwa nyingine.

Asili ya jina la Bungay linatokana na ardhi ya kabila moja liitwalo Bonna, lililokuwa linaishi pembezoni mwa Mto Waveney, Uingereza, na kusifika katika karne ya 13 kuwa na mchawi aliyeitwa Bongay. Tukio lile lilifanana na mchezo wa ligi ya Jumapili ya kriketi uliofanyika Uingereza 2014.

Wachezaji 22 wote wa kikosi cha timu ya Amarmian iliyocheza na Yorkshire katika mji wa Bradford walikuwa na jina la Patel. Tofauti ilikuwa ni  jina la kwanza. Kilichojulikana baadaye ni kwamba wachezaji sita katika kikosi hicho walikuwa ni wanafamilia moja. Kazi pevu waliipata watangazaji wa mchezo wa ma-Bungay, kwa vile walilazimika kueleza mpira anao Bungay, kampa Bungay, lakini Bungay wa timu ya pili ya Bungay amempokonya na kuupeleka upande wa pili wa Bungay.

Hiyo ni historia ya aina yake. Sasa, miaka 10 imepita, na watoto wa hawa ma-Bungay waliocheza ule mchezo, mashabiki wa mji wa Bungay wanataka ikiwezekana mwishoni mwa mwaka huu kuwa na tamasha kama lile lililofanyika 2016 ili kuonyesha heshima kwa wazee walioweka historia ya aina yake na wao kuweka historia yao.

Watoto hawa wa kiume na kike, ambao pia wana jina la Bungay wanakusudia kuwa na michezo miwili ya ma-Bungay, mmoja wa kandanda na mwingine wa netiboli katika uwanja mpya wa michezo wa nchi hiyo. Lakini, la ziada ni kwamba, kwa vile timu yao inaitwa Black Dogs, yaani Mbwa Weusi, basi pia watakuwa na kandanda la mbwa weusi. Miongoni mwa vigezo vya mbwa watakaoshiriki katika hilo pambano ni wale wenye umri wa zaidi ya mwaka mmoja na si zaidi ya mitano, na madaktari wa timu hizo wawe wale wa wanyama.

Hivi sasa wachezaji wa klabu hiyo wametakiwa kutafuta mbwa weusi na kuwafundisha kandanda na sheria zake. Mchezo wao utakuwa wa dakika 25, kila nusu ikiwa dakika 10 na mapumziko dakika tano. Waingereza hivi sasa wanausubiri kwa hamu mchezo huo ambao kama utachezwa, utafanyika katika uwanja wa mji huo ambao ulijengwa miaka iliyopita kwa gharama ya Pauni 547,803.

Mwamuzi na wasaidizi wake watakuwa ma-Bungay waliocheza ule mchezo wa kihistoria miaka ya nyuma, na fedha zitakazopatikana katika mchezo huo zitatumika kuwasaidia mayatima, watu wenye ulemavu na wasiojiweza wa mji huo. Vyombo vya habari vya Uingereza na nje hivi sasa vinagombania haki ya kuutangaza mchezo huo, na hii ni ishara ya kutokuwepo tatizo la kifedha za kutayarisha pambano hilo, ikiwa ni pamoja na kuwasafirisha kwa ndege wachezaji wenye jina la Bungay kutoka kila pembe ya dunia.

Mji wa Bungay huenda ukafurika wageni, na tayari panatayarishwa kuweka nyumba za mahema zaidi ya 500, kila moja ikiwa na vitanda vinne hadi sita kwa vile hoteli na nyumba za wageni zitajaa. Kinachosubiriwa ni hiyo siku na kama mkasa wa aina hiyo utashuhudiwa sehemu nyingine katika huu ulimwengu wa sasa, ambao mambo yake hayatabiriki kwa uhakika kama matokeo ya mchezo.