Kikoti ataja kilichomkwamisha msimu huu
Muktasari:
- Baada ya mapumziko ya kupisha kalenda ya michezo ya kimataifa, mechi ijayo ya Namungo FC itakuna dhidi ya TRA United. Mchezo huo utapigwa Oktoba 8, 2026, kuanzia saa 12:30 jioni.
MSIMU huu haujaanza vizuri kwa kiungo mshambuliaji wa Namungo, Lucas Kikoti, ambaye hadi sasa bado hajafungua akaunti yake ya mabao, wakati timu hiyo ikipambana kutafuta mwendo wa kujiweka salama kwenye mbio za Ligi Kuu Bara.
Namungo imecheza mechi saba katika msimu huu wa 2026-2027, ikishinda mbili na kupoteza tano, matokeo yaliyoifanya ibaki na pointi sita katika nafasi ya 13 kwenye msimamo. Kikosi hicho kimefunga mabao sita, lakini kimeruhusu 11, ikiwa ni tofauti ya mabao matano.
Akizungumza na Mwanaspoti Kikoti alikiri mwanzo wake binafsi haukuwa ule alioutamani, akifichua mapumziko marefu aliyopata nyumbani kabla ya kuanza kwa msimu yalimfanya arudi akiwa bado hajapata utayari ule alioutaka.
Amesema hali hiyo ilimlazimu kuanza kujitafuta tena ndani ya uwanja, huku akijipa muda wa kurejesha kiwango na kuingia kwenye kasi ya mashindano.
“Kiukweli msimu haujaanza vizuri kwangu. Nilipata mapumziko marefu zaidi nyumbani kabla ya msimu kuanza, hivyo niliporudi nilikuwa bado najitafuta. Lakini ninaendelea kujisukuma ili nirejee kwenye kiwango changu,” amesema Kikoti.
Licha ya kutokuwa amefunga bao hadi sasa, kiungo huyo hajakata tamaa, huku akitazama mbele zaidi na kuweka malengo yake binafsi sambamba na mahitaji ya timu.
“Nataka kuisaidia Namungo kupanda kwenye nafasi za juu zaidi katika msimamo, huku mimi mwenyewe nikiwa na shabaha ya kufikisha mabao saba mpaka 10 msimu huu,” amesema Kikoti.
Baada ya mapumziko ya kupisha kalenda ya michezo ya kimataifa, mechi ijayo ya Namungo FC itakuna dhidi ya TRA United. Mchezo huo utapigwa Oktoba 8, 2026, kuanzia saa 12:30 jioni.